Serikali imekipongeza Kituo cha Afya cha Makole kilichopo katika jiji la Dodoma kwa jitihada zake za kuboresha huduma za tiba, na kupelekea ongezeko kubwa la wateja kutoka 25,480 waliokuwa wakipata huduma kituoni hapo miezi mitatu iliyopita hadi 35,486 kufikia mwezi aprili mwaka huu sawa na ongezeko la wateja wapya 10,926 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 30.
Sambamba na ongezeko hilo, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita idadi ya wateja waliokuja kupata matibabu katika kituo hicho wanaotumia Bima ya Afya (NHIF) imeongezeka kutoka wateja 470 hadi 973 ambao ni karibu maradufu ya wateja waliokuwa wakipata matibabu katika kituo hicho.
Akizungumza na wafanyakazi wa kituo cha Afya Makole, wakati wa ziara yake ya pili kukitembelea kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt Dorothy Gwajima ameelezea furaha yake kufuatia kupokea taarifa ya kituo hicho na Mganga Mfawidhi Dkt George Matiko, ambayo imeonyesha kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya utoaji huduma kituoni hapo.
Dkt Gwajima amesema kuwa ikiwa ni miezi mitatu tangu alipofanya ziara yake kwa mara ya kwanza katika kituo hicho, mnamo Februari 17, mwaka huu, safari hii amefurahi kuona namna watendaji wa kituo hicho wakiongozwa na mlezi wa kituo hicho Bi Mary Shadrack walivyojidhatiti kutoa huduma bora za tiba kwa wananchi.
Amesema kitendo cha watumishi wa Kituo cha afya Makole kubadilika na kutoa huduma bora kwa wananchi kinapaswa kuigwa na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
“Nilipotembelea kituo hiki tarehe 17 Februari, 2019, nilikuta kituo chenu kikiwa na malalamiko mengi ya wagonjwa hasa kero ya foleni na malalamiko ya kutoa huduma mbovu kwa wagonjwa, lakini sasa mmebadilika hongereni sana,” amesema Dkt Gwajima na kuongeza:
“Napenda kuwasihi muendelee na ari hiyo ya kutoa huduma kwani wananchi wengi wangependa kupata huduma katika vituo vya afya vya umma lakini wanakatishwa tama na huduma na mazingira mabovu wanayoyakuta.”
Kufuatia mafanikio hayo ambayo yamepatikana katika kipindi kifupi, Dkt Gwajima ametaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini viige mfano wa kituo cha afya Makole.
Wakati huo huo Dkt Gwajima amewapongeza Makatibu Tawala wa mikoa ya Morogoro na Ruvuma kwa kufanyia kazi taarifa za ziara zake katika mikoa hiyo na matokeo yake viongozi hao kuamua kufanya mabadiliko kwa timu za usimamizi huduma za afya za mikoa yao jambo ambalo litaleta mabadiliko yatakayosaidia kuongeza kasi ya usimamizi kwa watendaji wapya watakaoteuliwa badala ya ule wa mazoea kama ulivyojidhihirisha kwa wajumbe walioondolewa.
Amesema katika mkoa wa Morogoro, katibu Tawala wa mkoa huo amelazimika kuwapumzisha wajumbe 9 wa Timu ya Uendeshaji Huduma za Afya Mkoa huo majukumu yao ya uongozi wa afya ili wakaendelee na majukumu ya kitaaluma katika vituo walivyopangiwa.
Wajumbe walioondolewa ni Dkt. Frank Jacob (Mganga Mkuu wa Mkoa) (RMO), Santiel Kinyongo (Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto) (RRCHCO), Salanga Maftah (Mratibu wa Huduma za Maabara) (RLT), na Florence Saka (Mratibu wa Malaria) (RMIFP).
Wengine ni Dkt. Emanuel Tenga (Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukimwi) (RTB/HIV), Leticia Nchia (Mratibu wa Huduma za Ukimwi) (RACC), Dkt. Samson Tarimo (Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno) (RDO), Grace Masawe (Muuguzi Mkuu wa Mkoa) na Dkt. Secondry Njau (Mratibu wa Afya ya Macho) (REC).
Aidha, Wajumbe wengine 6 wa Timu ya Afya Mkoa wa Morogoro wamepewa onyo la kuboresha utendaji wao vinginevyo nao watatolewa kwenye nafasi za uongozi mara moja. “Ukipewa nafasi ya uongozi wa afya ngazi ya mkoa na halmashauri usimamie, ufuatilie na uchukue hatua au utoke kwenye nafsi hiyo na siyo vinginevyo,” amesema Dkt Gwajima.
Pia Dkt Gwajima amesema Timu ya Usimamizi Huduma za Afya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma pia, wajumbe wake wote wa kudumu wameondolewa kwenye nafasi zao za uongozi kutokana na uwajibikaji wa mazoea.
Katika ziara hiyo, Dkt Gwajima aliongozana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt James Kiologwe na Mjumbe wa timu ya usimamizi na uendeshaji wa huduma za afya mkoa wa Dodoma Bi Mary Shadrack ambaye alipewa jukumu la kulea kituo hicho kwenye kipindi hiki cha maboresho.
Chanzo: tovuti ya OR-TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.