Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa Damu Salama, Dkt. Abdu Juma Bhombo amesema ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya kati Dodoma utaimarisha utoaji wa huduma za damu salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi wakati wa kujifungua katika Mikoa ya Dodoma, Iringa na Singida.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Oktoba, 2022 jijini Dodoma wakati wa ujio wa wadau wa maendeleo kutoka KOICA na UNICEF waliokuja kukagua maendeleo ujenzi wa kituo hicho.
Dkt. Juma amesema ujenzi wa kituo hiki cha kisasa unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu na kuanza kutoa huduma.
"Kituo hiki kitawezesha Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani kukusanya damu ya kufikia mahitaji ambapo mahitaji ya mkoa wa Dodoma ni chupa za damu zaidi ya laki 24,000 kwa mwaka", ameeleza Dkt. Juma
Aidha, ameeleza kukamilika kwa kituo hiki utawezesha Mkoa wa Dodoma kutengeneza mazao ya damu kama chembe sahani, Plasma (Fresh Frozen Plasma), ambayo ni mahususi kwa matibabu ya akina mama wanaojifungua na kumwaga damu nyingi na Chembe nyekundu kwa ajili ya matibabu ya Wagonjwa wanaopata upungufu wa damu.
Vile vile, Dkt. Juma ameongeza kuwa mazao hayo yataziwezesha hospitali za kanda kama Hospitali ya Benjamini Mkapa inayotoa huduma bobezi kama upandikizaji wa figo, kansa na matibabu mengine.
Hata hivyo amesema kituo kitawezesha upimaji sampuli za damu katika mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani na kuondokana na kupeleka sampuli mkoa wa Dar es salaam kwa ajili ya kupima maambukizi kwenye damu.
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya Kati Dodoma, Dkt. Katura Mathias amewashukuru wafadhili wa mradi huo ambao ni KOICA na UNICEF kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwa kujenga kituo cha kisasa cha Damu Salama Kanda ya Kati.
Dkt. Mathias amesema kituo hicho kitarahisisha upatikanaji wa majibu ya sampuli za damu salama kwa wakati na kufanya kituo hicho kuwa na damu ya kutosha kuwahudumia wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.