KATIKA kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwemo uporaji, ukabaji na udhalilishaji, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limedhamiria kujenga Kituo cha Polisi katika Kata ya Chang’ombe ambapo mpaka kukamilika kwake kinatarajiwa kugharimu Shilingi Milioni 130.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mshauri Mkuu wa Miradi ya Ujenzi ya Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Richard Malika wakati wa kupokea jumla ya matofali 6700 yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ikiwa ni jitihada za mkuu wa mkoa huyo kukabiliana na matukio ya uhalifu yaliyoshamiri katika Kata ya Chang’ombe huku Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikitoa kiasi cha Shilingi Milioni 10 katika kuchangia ujenzi huo.
“Tunakadiria hadi kukamilika kwa kituo hiki jumla ya Shilingi Milioni 130 zitakua zimetumika kama gharama yam ujenzi wa jengo ukiachana na samani za ofisi na kitakua kituo cha pili kwa ukubwa kwa hapa Dodoma sambamba na kuzingatia haki za binadamu huku kila mahabusu zikiwa na sehemu ya choo na mabomba ya maji” alisema Naibu Kamishna Malika
Naibu Kamishna Malika pia aliwataka wahalifu pindi kituo hicho kitakapokamilika watafute taratibu nyingine za maisha kwani uhalifu sio kazi nzuri huku akiweka wazi kituo hicho kitakamilka ndani ya miezi sita.
Akizungumza baada ya makabidhiano ya matofali hayo, Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira alisema wanaishukuru Wizara, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambae amechangia mifuko mia moja ya saruji katika mradi huo.
“Uhalifu hapa kwetu umekua ni changamoto watu wanaporwa wanafanyiwa matendo ya kihalifu lakini viongozi tumeanza mipango kukomesha uhalifu huo ikiwemo dhana ya ulinzi shirikishi na sasa ujenzi wa kituo hiki utaenda kukomesha matendo ya uhalifu katika maeneo ya Chang’ombe, sisi kama viongozi tutahakikisha tunawahamasisha wananchi wetu wachangie katika mradi huu na tunawashukuru wahisani wote waliotuunga mkono na wanaoendelea kutuunga mkono katika ujenzi huu”alisema Diwani Bakari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.