Kituo cha vyombo vya habari cha Dodoma Media Group kutoa elimu ya mpiga kura katika kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na utunzaji wa mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa na Mejena Mkuu wa Dodoma Media Group, Zania Miraji alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa kituo cha vyombo vya habari cha Dodoma Media Group kilichopo katika Mtaa wa Miyuji Proper jijini Dodoma kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024.
Miraji alisema “kupitia vyombo vya habari vya Dodoma Media Group jamii ya Dodoma itapata haki ya upatikanaji wa taarifa na elimu juu ya masuala mbalimbali ikizingatia ujumbe wa ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’. Elimu itakayotolewa ni pamoja na elimu ya masuala ya uchaguzi ikiwemo elimu ya mpiga kura ambapo kutakuwa na kipindi maalum cha kuelimisha Umma kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa. Pia itatolewa elimu juu ya lishe na kutakuwa na kipindi maalum kitakachozungumzia masuala ya lishe na elimu juu ya utunzaji wa mazingira na athari za uharibifu wa mazingira”.
Akiongelea lengo la mradi huo alisema kuwa ni kiunganishi muhimu kati ya sekta binafsi, serikali na jamii. Aliongeza kuwa mradi unaunga mkono jitihada za serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamishia shughuli za serikali na sekta binafsi mkoani Dodoma. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, mradi huu ukikamilika utatoa ajira kwa wafanyakazi 36 kati yao Wanaume 19 na wanawake 17 miongoni mwao watu wenye Ulemavu ni 03” alisema Miraji.
Akiongelea gharama za mradi, alisema kuwa hadi kukamilika utagharimu shilingi 1,000,000,000. Alisema kuwa hatua iliyofikiwa kiasi cha shilingi 700,000,000 kimetumika sawa na asilimia 70, akivitaja vyanzo vya fedha kuwa ni matangazo ya biashara, mkopo na mapato binafsi ya mkurugenzi.
Mradi wa kituo cha vyombo vya habari cha Dodoma Media Group ulianza kutekelezwa tarehe 1 Oktoba, 2018 ukitarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2024, ukihusisha ujenzi wa majengo ya studio za redio, televisheni, samani na mifumo ya umeme na maji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.