WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema, matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 yanaonesha kiwango cha uzingatiaji wa maadili kimefikia asilimia 75.9, hivyo kuongezeka kwa wastani wa asilimia 9.8 kikilinganishwa na cha asilimia 66.1 kinachotokana na matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka.2014.
Mhagama ametoa takwimu hizo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, na kuongeza kuwa matokeo hayo yanatokana na jitihada za kuimarisha uzingatiaji wa maadili chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhagama amesema, kutokana na dhamira thabiti ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka misingi imara ya usimamizi wa maadili ya kiutendaji kwa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Mhagama ameongeza kuwa, matokeo hayo pia yanatokana na ushirikiano na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la ukuzaji maadili, pamoja na utekelezaji mzuri wa Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na Rushwa.
Aidha, Mhagama amesema ofisi yake iliamua kutojitathmini yenyewe na badala yake kumpatia kazi ya utafiti Mtaalam Mwelekezi Dkt. Francis Mwaijande kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam ili afanye utafiti utakaokuwa na tija katika kuimarisha uzingatiaji wa maadili kwa watumishi wa umma.
"Tuliamua kumtafuta mtafiti huru kutoka nje ya ofisi yetu kwa lengo la kupata maoni na takwimu sahihi ya hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma" amefafanua Mhagama
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.