Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KATA ya Kiwanja cha Ndege inatekeleza ujenzi wa zahanati uliofikia hatua ya lenta ili kuwasogezea wananchi wake huduma za matibabu karibu na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma hizo mbali.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Ashura Iberi mbele ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa zahanati hiyo mwishoni mwa wiki.
Iberi alisema kuwa kata yake ilipokea shilingi 40,000,000 kwa awamu tatu kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Alisema kuwa awamu ya kwanza walipokea shilingi 10,000,000 zilizotumika kuseti jengo, kuchimba msingi, kumwaga zege la awali la msingi na kujenga tofali za msingi. “Awamu ya pili ilipokea shilingi 10,000,000 zilizofanya kazi ya kujaza kifusi, kupanga mawe, kusuka nondo na kumwaga zege la jamvi. Kazi nyingine ni kujenga ukuta wa kozi 10 na kufunga mbao za pembezoni mwa jamvi na utandazaji wa DPM, kufukia, kuondoa mbao na kumwagilia maji” alisema Iberi.
Kaimu Afisa Mtendaji huyo alisema kuwa awamu ya tatu walipokea shilingi 20,000,000 zilizotumika kununua vifaa vya ujenzi na kumlipa fundi. “Kazi zilizobaki ni kupaua, kutengeneza mfumo wa maji safi na taka, kuchimba bomba za umeme, kufitisha madirisha, kupiga plasta, blundering na kufunga bodi, skiming, kutengeneza sakafu ya kupokea vigae, rangi na kufunga milango na vitasa” alisema Iberi.
Mtendaji huyo alimshukuru Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma na Kamati yake ya Fedha na Utawala kutembelea na kukagua ujenzi huo. “Tunatoa shukrani pia kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na Mhandisi Nicodemus Kileo kwa kutupatia ushirikiano wa karibu katika kazi zote zinazoendelea. Pia Diwani na Kamati ya Maendeleo ya Kata, Kamati ya Manunuzi, Mapokezi na Ujenzi na watendaji wote wa mitaa na wataalam kwa ushauri na usimamizi mzuri” alisema Iberi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliagiza iandaliwe ‘BOQ’ itakayoonesha gharama ya mradi wote hadi utakapokamilika. Alisema kuwa ‘BOQ’ itaiwezesha halmashauri kujua kiasi cha fedha kinachohitajika ili kinapotolewa kiwe na tija zaidi.
Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilifanya ziara ya kikazi kiutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na jiji hilo kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili-Juni, 2022).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.