KIKOSI cha Dodoma Jiji FC leo kimefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Coastal Union kutoka Tanga, mchezo utakaochezwa katika dimba hilo kesho Jumatano ya tarehe 17 Februari na mchezo utaanza saa 8:00 mchana.
Akizungumza na mwandishi wetu Kocha mkuu wa timu hiyo Mbwana Makata amesema kuwa mechi hiyo ni muhimu sana kwao na bechi la ufundi pamoja na wachezaji wanalijua hilo hivyo wanaingia kwenye mchezo huo kupambana ili waweze kuondoka na pointi tatu.
Makata amesema kuwa yapo mapungufu aliyoyaona katika mchezo uliopita licha ya kushinda katika mchezo huo ambapo changamoto kubwa ilikua ni kwenye eneo la ulinzi na umaliziaji hivyo yeye pamoja na benchi la ufundi wamelifanyia kazi ili lisiweze kujitokeza katika mchezo wao dhidi ya Coastal Union.
“Coastal Union ni timu bora na imetoka kupata matokeo mazuri dhidi ya Azam kwa hiyo naamini watakuja kwa kasi ya hali ya juu ili waweze kushinda, na sisi tumeliona hilo tutacheza kwa tahadhali kubwa na kuzitumia nafasi zote tutakazopata ili tuweze kutoka na matokeo mazuri” alisema Makata.
Aidha amesema kuwa wachezaji waliokua majeruhi kama vile Rajab Mgalula, Omari Daga na Santos Thomas wote wameanza kufanya mazoezi ya kawaida na kikosi hivyo anaamini wanaweza wakacheza katika mchezo wa kesho.
Huu ni mchezo wa pili wa Dodoma Jiji FC dhidi ya Coastal Union ambapo katika mchezo uliopita walitoka sare ya bila kufungana katika dimba la Mkwakwani Jijini Tanga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.