MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kwa ulipaji wa kodi ya majengo kupitia manunuzi ya mfumo wa LUKU kuanzia kesho, Ijumaa Agosti 20, 2021 pamoja na viwango vipya kulingana na majengo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo kwa sasa walio na nyumba za kawaida ndani ya kiwanja kimoja watalipa Shilingi 12,000 badala ya Shilingi 10,000 iliyokuwa ikitozwa awali na Shilingi 60,000 kwa kila sakafu ya ghorofa kutoka Shilingi 50,000.
Aidha, kwa upande wa Halmashauri za Wilaya na Miji Midogo wao pia wataguswa na ongezeko hilo licha ya kuwa na ahueni kwani watalipa Shilingi 60,000 kwa nyumba za ghorofa bila kujali idadi ya sakafu.
Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata (pichani) ameeleza katika taarifa yake leo kuwa utekelezaji huo unafanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ukihusisha mita za aina zote za umeme.
“Hili linafanyika kufuatia marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sura ya 289 iliyopitishwa na Bunge la Bajeti la mwaka 2021 ambapo viwango vya kodi ya majengo vimebadilishwa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa njia hii mpya ya ukusanyaji wa kodí, kíla mnunuzi wa umeme atakatwa Shilingi 1,000 kwa mwezi kwa nyumba ya kawaida na Shilingi 5,000 kwa mwezi kwa kila sakafu ya ghorofa.
"Kwa wale wanaotumia mita za Ankara watalipa kodi hii kwa pamoja katika Ankara ya mwezi. Kwa wamiliki ambao majengo yao hayajapata umeme, wataendelea kulipa kodi hiyo kwa kutumia mfumo uliokuwa unatumika hapo awali ambao ni njia ya simu ya mkononi na benki baada ya kupata namba ya kulipia malipo (Control Number) mpaka hapo watakapoingiziwa umeme.
Wamiliki wa majengo na wananchi kwa ujumla watakaokatwa kodi hiyo kimakosa na wale watakaokuwa na malalamiko mbalimbali, watatakiwa kufika katika ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao kwa ajili ya kushughulikiwa."
Hapo awali Kodi ya Majengo ilikuwa ikikusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kabla ya mwaka 2016/17 jukumu hili kuhamishiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na hadi sasa inaendelea kusimamia jukumu hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.