TAASISI ya Maendeleo ya Vijana Dodoma imepongezwa kwa kupambana kikamilifu na masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wasichana katika kupunguza na kutokomeza mimba za utotoni.
Hayo yamesemwa jana na Mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Mhe. Dkt. Binilith Mahenge ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga. Maadhimisho hayo yaliambatana na kauli mbiu isemayo “Tupinge ukatili wa kijinsia; mabadiliko yanaanza na mimi”.
“Naipongeza sana Taasisi ya DOYODO kwa kupambana kikamilifu na masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wasichana hasa katika kupunguza na kutokomeza mimba za utotoni hapa jijini Dodoma” alisema Mhe. Maganga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO ndugu Rajabu Juma Suleiman aliongea wakati wa maadhimisho hayo aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kutambua jitihada zinazofanywa na SHirika la DOYODO na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na wadau mbalimbali kwenye masuala ya maendeleo ya vijana jijiini Dodoma na kwa taifa zima kwa ujumla.
Aidha, Mkurugenzi Rajabu aliwapongeza vijana wa DOYODO kwa kutimiza miaka mitano ya kishindo tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo maarufu sana Jijini Dodoma.
Akifafanua zaidi kuhusu DOYODO Rajabu alisema kuwa, taasisi hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2014 ikiwa kama Umoja wa Vijana Dodoma (UWAVIDO) ambapo ilianza na vijana wasiopungua 40. Mwaka 2015 ilisajiriwa kisheria kama taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) na kuwa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana mkoani Dodoma (DOYODO).
Tangu kuanzishwa kwake DOYODO imekuwa na lengo la kuwajengea vijana uwezo kwenye maeneo ya elimu, uchumi, afya na uongozi, vilevile imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha vijana wananufaika na fursa mbalimbali za maendeleo katika Mkoa wa Dodoma. Vijana walengwa ni wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 24 ikijumuisha vijana waliopo mashuleni na hata nje ya shule. Katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake DOYODO imefanikiwa kuanzisha na kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo mabinti ili waweze kutimiza ndoto zao, mradi huo unaitwa “Magauni Manne Girls Empowerment Project”.
Mkurugenzi Mtendaji Rajabu alisema hivi sasa taasisi hiyo ina vijana takribani 130 ambao wanatoka katika vikundi vya vijana kwenye kata na mashuleni na taasisi ina viongozi saba hivi sasa.
Picha na matukio mbalimbali:
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Josephat Maganga aliyemwakilisha Mgeni Rasmi Dkt. Binilith Mahenge akikabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO cheti cha heshima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Dkt. Binilith Mahenge ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake wa kuwasaidia vijana kunufaika na fursa zilizopo mkoani Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO Rajabu Suleiman aliyesimama wakati akielezea kuhusu DOYODO na maendeleo ya Mradi wa Magauni Manne.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.