KONGAMANO la Maafisa na Wadau wa Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania limefanyika Jijini Dodoma na kufunguliwa na mgeni rasmi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima.
Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Mkoani Dodoma (DOYODO) Ilipata fursa ya Kushiriki Kongamano na kuonesha shughuli na miradi inayoendeshwa na taasisi hiyo ya vijana iliyojizolea umaarufu mkubwa Jijini Dodoma kwa mikakati na utekelezajiwa wa majukumu yake.
Aidha, Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akiwa ameambatana na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Vijana wa Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipata fursa ya kutembelea banda la DOYODO ambapo Afisa Mjengea uwezo wa DOYODO, Hawa Said alimuelezea mgeni rasmi kuhusu Mradi wa Magauni manne unaolenga kutokomeza mimba za utotoni jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipongeza sana mradi huo pamoja na kuvutiwa na namna ambavyo DOYODO imekuwa kinara wa kupambana na mimba za utotoni mkoani Dodoma, lakini pia aliahidi kutembelea Ofisi za DOYODO kwa lengo la kuendelea kuboresha ushirikiano hususani kwenye mapambano ya mimba za utotoni na ukatili kwa watoto wa kike.
Vile vile, Waziri alikagua bidhaa za vikundi vilivyokopeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kupongeza jitihada zinazofanywa na Jiji la Dodoma kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa vitendo agizo la kutenga na kutoa mikopo ya asilimia kumi (10%) kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (wa pili kushoto) akimsikiliza kwa makini Afisa Mjengea uwezo wa DOYODO Hawa Said (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kuhudu mradi wa Magauni Manne unaoendeshwa na Taasisi ya DOYODO. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Vijana wa Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang'anya.
Chanzo: Idara ya Habari na Mawasiliano DOYODO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.