Na. Theresia Nkwanga, DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuing’arisha Dodoma kimiundombinu ikiwa na mtandao mrefu wa barabara za lami na kuchochea maendeleo katika Jiji la Dodoma.
Pongezi hizo alizitoa katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujadili mapendekezo ya mpango wa Bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika ukumbi wa mikutano wa Jiji la Dodoma.
Mavunde alisema kuwa Dodoma ni kati ya maeneo ambayo kwa kiwango kikubwa yameguswa na barabara ya lami. Dodoma Jiji inaongoza Tanzania nzima kwa kuwa na mtandao mrefu wa barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 194.8 ikifuatiwa na Manispaa ya Kinondoni yenye barabara zenye urefu wa Kilometa 177.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwakutujengea miundombinu ya barabara. Tunaamini kazi hii itaendelea na Dodoma itazidi kupaa na kung’ara zaidi” alisema Mavunde.
Aidha, aliwashauri Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Wilaya ya Dodoma (TARURA) kujikita zaidi katika kutengeneza kilometa chache za barabara kwa ukamilifu kuliko kufanya matengenezo kwa ukubwa wa kilometa mvua zikinyesha barabara zinaharibika hivyo, kuhitaji matengenezo mengine.
“Kila mwaka tunazitengea fedha lakini zinarudi katika utaratibu uleule kwanini msibadilishe utaratibu badala yakuwa na barabara ya kilometa 10 yenye bajeti ya kilometa 10 kwaajili ya kwenda kukwangua barabara, kwanini msiifanye ikawa kilometa tano, ikatengenezwa kwa ukamilifu ikatumika muda wote mkamalizia kipindi kingine kuliko kutumia fedha ya kilometa 10 kukwangua barabara mvua zikinyesha barabara zinaharibika mnaanza upya” alisema Mavunde.
Naye, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe, alisema kuwa TARURA katika mwaka wa fedha 2023/2024 imejipanga kutengeneza kilometa 483.4 sawa na asilimia 40 ya kilometa zote za Jiji la Dodoma. Alisema kuwa bajeti hiyo itahusisha matengenezo ya kawaida, ya muda maalumu na maeneo korofi.
“Ukiangalia bajeti yetu kwa haraka kuna takribani kilometa 483.4 zinazoenda kutengenezwa wakati ukiangalia mtandao wetu una kilometa 1,180 zile ambazo zinatambulika na TARURA. Kilometa 696 sawa na asilimia 60 haziguswi kabisa pamoja na kwamba bajeti imeongezeka bado tunachangamoto ukizingatia ukuaji wa kasi wa Jiji la Dodoma. Tunatakiwa kuongeza vyanzo vya mapato ili kuhakikisha mtandao wa barabara tunaweza kuhudumia kwa asilimia kubwa,’’ alisema Mhandisi Kilembe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.