WANAWAKE waliofungwa katika gereza la Isanga wana mahitaji kama wanawake wengine katika jamii na kustahili upendo na kuthaminiwa ili wafurahie maisha wawapo gerezani na watakapotoka nje ya gereza.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Honoratha Rwegasira muda mfupi kabla ya kamati ya maandalizi ya siku ya wanawake Mkoa wa Dodoma kwenda kutembelea wanawake waliofungwa katika gereza la Isanga na kituo cha wa watoto yatina na wazee Hombolo leo.
Honoratha amesema kuwa katika kuelekea kilele cha siku ya wanawake, kamati ya maandalizi imepanga kwenda kutembelea na kutoa misaada kwa wafungwa wanawake katika gereza la Isanga. Akiongelea sababu za kutembelea wafungwa wanawake waliofungwa katika gereza hilo, amesema “Wafungwa hao ni wanawake wenzetu. Wapo waliofungwa kwa makosa mbalimbali na magereza ni sehemu ya kujifunza.
Hivyo, kwenda kwetu kuwatembelea ni kuonesha upendo wetu kwao na kuwakumbusha kuwa hawajatengwa na jamii. Tunavyoenda wao watajifunza kutoka kwetu na wapo watakaohitaji msaada kutoka kwetu”.
Alisema kuwa katika timu hiyo atakuwepo afisa ustawi wa jamii ili kama kuna wafungwa wenye watoto wadogo waone jinsi ya kuwasaidia watoto hao ili wasiwe sehemu ya kutumikia vifungo vya mama zao.
Akiongelea kituo cha watoto yatima na wazee Hombolo, Afisa Maendeleo ya Jamii huyo alisema kuwa ziara hiyo inalenga kwenda kuwafariji watoto na wazee katika kituo hicho.
Kuhusu misaada itakayopelekwa aliitaja kuwa ni nguo mbalimbali, sabuni za kufulia na kuoga, mafuta ya kula na kupaka na taulo za kike. Zawadi nyingine ni maziwa, mchele, sukari, chumvi na unga, pampasi pamoja na misaada mingine.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa Mkoa wa Dodoma kitafanyika katika shule ya msingi Mkonze, mgeni rasmi atakuwa mama Felista Bura, Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Dodoma. Maadhimisho mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kizazi cha usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.