Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma amepongeza ubunifu wa wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari katika kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kipindi hiki cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji Godwin Kunambi wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri jana kuhusu mkakati wa Halmashauri ya Jiji kuendelea kuwafundisha wanafunzi katika kipindi cha mapumziko.
Kunambi alisema “pongezi kwa wakuu wa Idara ya elimu msingi na sekondari wa Halmashauri ya Jiji kwa ubunifu huu wa kuwafundisha wanafunzi kupitia redio za Dodoma na mitandao kipindi hiki cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya corona”. Halmashauri ya Jiji la Dodoma inazo shule za msingi 133 zenye jumla ya wanafunzi 113,441 na shule za sekondari 56 zenye wanafunzi 30,785, aliongeza. “Ndugu waandishi wa habari mtaona idadi hii kubwa ya wanafunzi wapo nyumbani. Changamoto kubwa ni uzururaji wa wanafunzi mitaani kwa sababu hawana kazi za kufanya nyumbani. Sasa tumekuja na jawabu la kuwafanya wasizurure. Tumewaandalia vipindi katika redio za Dodoma na mitandao ya kijamii” alisema Kunambi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kipindi hiki watajikita katika kufundisha madarasa yanayofanya mitihani ya kitaifa. Aliyataja madarasa hayo kwa elimu ya msingi kuwa ni darasa la nne na la saba na kwa elimu ya sekondari kidato cha pili na cha nne. “Napenda kuwapongeza walimu wote wa shule za msingi na sekondari waliojitolea kuandaa vipindi kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi kipindi hiki cha mapumziko. Kazi wanayofanya ni nzuri na ya heshima kubwa kwa Halmashauri yetu ya Jiji la Dodoma.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Upendo Rweyemamu alisema kuwa katika vipindi vitakavyofundishwa ni masomo yote ya kidato cha pili na cha nne. Walimu wabobezi 26 wameandaliwa na ratiba ya vipindi hivyo itawekwa katika tovuti ya Halmashauri, aliongeza.
Nae Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma, Mwl. Joseph Mabeyo alisema kuwa walimu wameandaliwa vizuri na mada zipo tayari kwa ajili ya wanafunzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.