Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amelishauri Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania kutokana na ushirikiano ambao amekuwa akiwapatia katika kutekeleza majukumu yao jana ofisini kwake.
Kunambi alisema “nataka makao makuu ya Machinga yawe jijini Dodoma. Tutaanza na kutafuta ofisi hapahapa Dodoma”, alisema Kunambi. Vilevile, aliwashauri kuangalia uwezekano wa kufanya mkutano wa Machinga Tanzania katika Jiji la Dodoma. Mkutano huo ni vizuri ukawa na utoaji wa elimu kuhusiana na masuala mbalimbali kwa Machinga, aliongeza. Katika kuonesha shukrani kwa Rais Dkt. John Magufuli kwa mapenzi yake kwa Machinga, ni vizuri mkamualika kufungua mkutano huo.
Mkurugenzi wa Jiji aliwataka Machinga kufanya shughuli zao na kukua kimtaji. “Lazima tuwe na mpango wa kufanya mabadiliko kutoka Machinga kwenda kuwa wafanyabiashara. Hata Mbuyu ulianza kama mchicha” alisema Kunambi. Aliushauri umoja huo kuangalia uwezekano kwa kuanzisha vitega uchumi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hoteli na majengo.
Katika kuhakikisha Machinga wanafanya kazi zao vizuri, Mkurugenzi huyo alisema kuwa Jiji la Dodoma linataka kufanya Machinga wa kisasa. Machinga wanaofanya kazi zao vizuri kwa kuzingatia taratibu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania, Ernest Masanja alisema kuwa umoja huo umeona vizuri kumpa cheti cha shukrani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutokana na ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa Machinga katika kutekeleza majukumu yao na jinsi ambavyo amefanikisha zoezi la ugawaji vitambulisho vya wajasilimali. Akiongelea ushauri wa Mkurugenzi wa makao makuu ya Machinga kuhamia Dodoma, alisema wapo tayari. “Kwa kuwa kipenzi chetu Rais, Dkt. John Magufuli anahamia Dodoma na sisi tupo tayari kuhamishia makao makuu ya machinga Dodoma” alisema Masanja.
Jiji la Dodoma ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimemaliza kuuza vitambulisho vyote walivyopewa kwa ajili ya kuwauzia wafanyabiashara wadogo. Vitambulisho 15,173 vya wajasiliamali vimeshauzwa kwa wafanyabiashara kwa bei ya shilingi 20,000 kwa kila kimoja.
Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania Ernest Masanja akimkabishi cheti Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi ofisini kwake jana.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (katikati) akiwa na viongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania walipomtembelea ofisini kwake jana.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi akiongea na timu ya uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga waliomtembelea ofisini kwake jana na kujadiliana mambo mbalimbali ya maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.