MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amewatoa hofu wananchi kuwa hakuna aliyepewa kibanda cha biashara katika maeneo ya stendi kuu ya mabasi, soko kuu la Job Ndugai na eneo la bustani ya mapumziko ya Chinangali badala yake taratibu za upangishaji zitatangazwa wazi.
Kunambi alisema hayo katika bustani ya mapumziko ya Chinangali wakati wa kuhitimisha ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ya kukagua ukamilishaji wa miradi ya kimkakati ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi Kunambi alisema “kumetokea na sintofahamu. Kuna watu wameibuka huko mtaani kama madalali wao wanasema tupe chochote tutakusaidia kupata kibanda eneo la ‘bus terminal’ na eneo la soko kuu la Job Ndugai na eneo hili la bustani ya mapumziko Chinangali. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, napenda kukuhakikishia kuwa mpaka sasa hivi hakuna mwananchi yeyote aliyepewa kibanda. Inasemwa mtaani kuwa hakuna haja ya kuomba wameshapeana, hiyo lugha si nzuri”.
Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa kimeundwa kikosi kazi kwa ajili ya kuratibu upangishaji wa miradi hii yote. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kwenye kikosi kazi hicho, katika kuimarisha na kuboresha uwazi ndani ya kikosi kazi kuna watu wa TAKUKURU ambao wataangalia zoezi na mchakato mzima ili rushwa isipewe nafasi” alisema Kunambi.
Mkurugenzi huyo aliwataarifu wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla kuwa hiyo ni fursa kwao. “Kwa Wana-Dodoma na watanzania kwa ujumla hii ni fursa kwenu kuja kuwekeza. Yeyote mwenye uwezo wa kufanya biashara eneo la stendi kuu ya mabasi, kufanya biashara eneo la soko kuu la Job Ndugai na kufanya biashara eneo la bustani ya mapumziko ya Chinangali achangamkie fursa hiyo” alisema Kunambi.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alitembelea stendi kuu ya mabasi, soko kuu la Job Ndugai na bustani ya mapumziko ya Chinangali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.