SERIKALI imezungumzia kupanda kwa bei ya vyakula nchini hususani nafaka. Imesema hali hiyo imetokana na serikali kuondoa ukiritimba, kwa kuruhusu ushindani katika uuzaji mazao ya kilimo.
Hata hivyo, imetoa matumaini kwamba pamoja na ongezeko la mahitaji hususani ya mahindi ndani na nje ya nchi kuchangia bei kupanda, miezi michache ijayo itashuka, kwani wakulima wataanza kuvuna mashambani. Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalumu juu ya hali halisi ya kupanda kwa mahindi, unga, mchele, maharage katika maeneo mbalimbali nchini
“Awali tulizuia mazao yasiuzwe nje ya nchi. Tunapofungua mipaka kuuza nje ya nchi, ushindani umechukua nafasi ndiyo sababu ya bei kupanda. Lakini ikifika Februari bei itashuka, mazao yataanza kutoka mashambani,” alisema Bashe.
Alisema mahitaji ya mahindi, yamekuwa makubwa siyo tu nchini, bali pia kwa nchi zinazozunguka Tanzania.
“Ni fursa kwa wakulima. Naendelea kuhamasisha wakulima zalisheni kwa kiwango chochote mnachoweza, hakuna wa kuingilia soko lenu, wapi na bei gani muuze” alisema.
Akisisitiza msimamo wa serikali wa kutoingilia bei ya mazao ya wakulima, Bashe alisema bei inayoonekana sasa, ndiyo thamani halisi ya mkulima. “Hatutaingilia kupunguza bei ya mazao. Wakati unajiuliza swali la bei kupanda, jiulize mwaka jana mkulima alikuwa ananunua saruji au bati kwa bei gani?
“Tulijenga utamaduni wa kuingilia na kumdhibiti mkulima. Akilima ni zao lake binafsi, lakini akivuna linageuka kuwa mali ya umma. Bei imepanda kwa sababu tumeruhusu soko lichukue nafasi yake na bei inatokana na demand and supply,” alifafanua Bashe.
SOKO NCHI ZA NJE
Kwa mujibu wa Bashe, mahitaji ya mazao yamekuwa makubwa ndani na nje ya nchi. Miongoni mwa nchi ambazo zimeanza kununua mahindi nchini ni Zimbabwe kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Burundi na Rwanda kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB). Pia wafanyabiashara binafsi, wameachiwa uhuru wa kuuza nje ya nchi.
Akizungumzia mahitaji ya mahindi, naibu waziri huyo alisema wigo umepanuka, kwani awali yalichukuliwa kama ni zao la chakula cha binadamu tu, lakini sasa yanatumika pia kama chakula cha wanyama na kuku.
Akieleza serikali inavyohakikisha wakulima wananufaika na si wafanyabiashara pekee, Bashe alisema inawapa taarifa sahihi, kwa kuwaambia bei halisi ya mazao kwenye masoko, kama vile jijini Dar es Salaam kisha wao wanaamua.
NFRA na CPB ambazo ni taasisi za serikali, pia zinapokwenda kununua mazao kwa wakulima, zinatoa bei shindani, ambayo inafanya pia wafanyabiashara kutoa bei iliyo nzuri zaidi. Bei ilivyopaa Jijini Dar es Salaam, kiroba cha unga wa sembe cha kilogramu tano, ambacho takribani miezi mitatu iliyopita kilikuwa kikiuzwa kati ya Sh 5,000 na 6,000, sasa kinauzwa Sh 8,000.
Mchele ambao kilogramu iliuzwa kati ya Sh 1,500 na 2,000 kulingana na kiwango chake, sasa unauzwa kati ya Sh 1,700 na 2,200. Katika maeneo yanayozalisha mazao ya chakula kwa wingi mfano Rukwa, imebainika mjini Sumbawanga na mji wa Namanyere wilayani Nkasi, bei ya na mahindi imepanda maradufu.
Mfanyabiashara wa nafaka anayemiliki ghala la nafaka (Mwanafyale Store) mjini Sumbawanga, Bukuku Mwanafyale alisema gunia la mahindi lenye kilogramu 100 ambalo lilikuwa likiuzwa Sh 18,000, sasa linauzwa kati ya Sh 96,000.
Mjini Namanyere bei ya mahindi imepanda kutoka Sh 30,000 kwa gunia lenye kilogramu 100 hadi Sh 84,000. Bei ya mchele imepaa kutoka Sh 1,500 kwa kilogramu hadi Sh 2,000.
“Debe la mahindi lenye ujazo wa lita 20 lilikuwa likiuzwa shilingi 5,000 miezi michache iliyopita lakini sasa linauzwa shilingi 14,000,” alisema mkazi wa Nkasi, John Nusurupia. Mjini Sumbawanga bei ya rejareja ya mchele, imeporomoka kutoka Sh 2,300 hadi kati ya Sh 1,500 na 1,700 kwa kilo kulingana na ubora wake. “Mara nyingi kila msimu bei ya mahindi ikipanda basi bei ya mchele inaporomoka,” alisema mchuuzi wa mchele, Semeni Ally.
Kutoka Mkoani Tanga, imebainika kuwa licha ya wakulima wa mahindi wa wilaya za Muheza, Mkinga, Handeni, Korogwe na Kilindi kuvuna mahindi, baadhi ya wafanyabiashara wa mahindi bado wanauza bei kubwa, ambapo gunia moja lenye uzito wa kilogramu 100 linauzwa kati ya Sh 70,000 hadi Sh 80,000.
Mfanyabiashara wa mahindi katika soko la mahindi la Ngamiani na Barabara 15 jijini Tanga, Juma Ally alisema “Kwa sasa hali ya mazao kama mahindi yamepanda bei sana ambapo gunia moja la mahindi tunauziwa na wakulima kwa kati ya shilingi 65,000 na 70,000, tunapoyasafirisha hadi kwenye soko na sisi ili tupate faida tunauza kati ya shilingi 70,000 hadi 80,000 kwani bila kufanya hivyo hatuwezi kupata faida”.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakulima wa mahindi kutoka wilaya za Muheza, Kilindi, Korogwe na Mkinga walimpongeza Rais Dk John Magufuli, kwa kutambua mchango na juhudi kubwa zinazofanywa na wakulima, kwani kwa muda mrefu wakulima walikuwa wakilanguliwa na wafanyabiashara wakubwa.
Kenedy Massawe, mkulima wa mahindi Wilaya ya Korogwe alisema baadhi ya wakulima wa mahindi, walikuwa hawanufaiki na zao hilo kutokana na wafanyabiashara kutoka Kenya kuja kwa wakulima na ‘kuchumbia’ mahindi yangali shambani, hivyo mkulima alikuwa hanufaiki na kilimo hicho.
Ufafanuzi wa Naibu Waziri, Bashe, kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula, hautofautiani na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliowahi kutoa mwaka jana, akisema hakuna uhaba wa chakula isipokuwa mahitaji ya soko, ndiyo yameongezeka na kusababisha bei kupanda.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.