Na. Josephina Kayugwa, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kwa kuwataka kuhakikisha wazee wanalindwa na wanakuwa salama kwa lengo la kuondokana na tatizo la ukatili linaloendelea.
Wito huo ameutoa katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Mashujaa Jijini Dodoma yakiongozwa na kauli mbiu inayosema "Ustahimilivu na mchango wa wazee ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa".
"Wazee wamekuwa wakikutana na changamoto hasa tatizo la ukatili limekuwa likiwakumba sana na kutishia usalama wa maisha yao, wengine wamekuwa wakiuawa kutokana na imani zisizofaa katika jamii kitu ambacho sio kizuri kabisa.
Sisi sote tuna jukumu la kuwalinda na kuwathamini hawa wazee kutokana na mchango mkubwa wa kimaendeleo ambao ulifanywa na wao, hivyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wananchi wote tuhakikishe tunawalinda wazee." amesema Simbachawene.
Akifafanua zaidi Simbachawene amesema suala la kuwalinda na kuwathamini wazee linaanzia katika ngazi ya familia kwanza, kwasababu huko ndiko taarifa zao zinapatikana kiusahihi na kama ushirikiano ukipatikana kutoka huko basi wazee hawa watakaa kwa amani.
Aidha waziri Simbachawene aliwaomba wadau wengine kuungana na serikali katika kuwasadia wazee katika mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula, mavazi na maradhi lakini pia Halmashauri zote ziangalie utaratibu wa kuwatambua wazee katika kila eneo husika kwa kuwapatia bima zitakazowasaidia katika matibabu.
Kwa upande wake Abdul Kikoo, mkazi wa Makole Jijini Dodoma ameishukuru Serikali kwa kuona mchango wa wazee katika Taifa kwa kuwawekea siku maalumu ya kuwakumbuka na kukumbushana kama jamii juu ya umuhimu wa kuwathamini na kuwalinda wazee.
"Nipende kusema asante kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutukumbuka, kwa karne hizi vijana baadhi yao wamekuwa hawawathamini wazee kiasi cha kuwafanyia ukatili mbaya hata kuondoa uhai wa wazee.
Tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii hasa vijana ambao wengi wao wameonekana kutokuwa na maadili kwa kutofuata utamaduni wa kitanzania, kitu kinachosababisha kuvunjika kwa sheria na utaratibu," alisema Kikoo.
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 14 Disemba, 1990 Umoja wa Mataifa uliridhia na kusema kwamba tarehe 1 Oktoba kila mwaka itakuwa siku ya wazee kimataifa, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwathamini wazee kwa mwaka huu imeadhimisha siku ya wazee kitaifa tarehe 3 Octoba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.