MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka amepokea taarifa ya makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa Dkt. Binilith Mahenge aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Hafla ya makabidhiano ya Ofisi hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita tarehe 21 Mei, 2021 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kuhudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi zilizopo Mkoani Dodoma, Viongozi wa Dini na wawakilishi wa Wazee wa Mkoa wa Dodoma.
Dkt. Binilith Mahenge amewataka Viongozi Mkoani Dodoma kumpa ushirikiano wa karibu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kama walivyofanya kwake.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mahenge alisema, mafanikio ya kazi kubwa aliyoifanya akiwa Dodoma yamesababishwa na ushirikiano wa karibu baina yake na viongozi wengine hivyo amewaomba kuendelea kutoa ushirikiano huo kwa Mhe. Mtaka.
"Nawaomba sana viongozi wenzangu, jinsi mlivyonisaidia mimi mfanye hivyo hivyo kwa Mtaka, anawategemea sana katika kutekeleza jukumu la kuleta maendeleo;
Naondoka mimi kama mimi nawaacha, naondoka nikiwa na huzuni kwa sababu nawaacha watu waliokuwa na mimi bega kwa bega, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya ushirikiano," alisema Dkt. Mahenge kwa hisia.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida alitumia nafasi hiyo kumtoa wasiwasi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa yupo tayari kushirikiana naye hata kwa kusafiri pale anapohitaji msaada wake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka alimuelezea Dkt. Mahenge kuwa ni kiongozi makini mwenye haiba ya uongozi huku akiahidi kuuenzi uongozi wake na yale aliyoyaacha Dodoma.
“Pamoja na Mahenge kuondoka Dodoma, kamwe hawezi kufanana na baadhi ya viongozi ambao hutumia fursa ya uhamisho wa viongozi wenzao kujitukuza na kuibua upya migogoro iliyokwisha tatuliwa” alisema Mhe. Mtaka.
Aliongeza kuwa hilo tatizo ndilo ambalo limekuwa likichochea migogoro ya ardhi na kusababisha migongano kwenye jamii.
"Kuna migogoro mingi ya ardhi imeshindwa kufikia muafaka kutokana na unafiki wa baadhi ya viongozi, mwenzake akiondoka au kuhamishiwa sehemu nyingine yeye anaanza upya kuibua migogoro ili mwenzake aonekane hakufanya lolote;
Tabia hii ni mbaya, sisi wote ni kitu kimoja tupo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi" alimalizia Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.