JAMII imeshauriwa kulima zao la Kitunguu kutokana na kutokuwa na usumbufu wakati wa kilimo chake na kutoa matokeo mazuri kiuchumi kwa mkulima.
Kauli hiyo ilitolewa na bwana shamba kutoka JKT Makutopora, Gabriel Maganga alipokuwa akitoa elimu ya kilimo cha zao la kitunguu katika banda JKT lililopo katika maonesho ya Nanenane eneo la Nzuguni Jijini hapa.
Maganga alisema kuwa kilimo cha zao la Kitunguu ni moja ya kilimo chenye faida kubwa kwa mkulima hasa akifuata vizuri kalenda ya kilimo. Kalenda ya kilimo huanza mwezi Julai na maandalizi ya shamba ikifuatwa na matukio mengine kwa mujibu wa ushauri wa wataalam.
Akiongelea mavuno, Maganga alisema kuwa vitunguu hukomaa kwa muda wa miezi mitatu na nusu mpaka minne na nusu tangu kusia mbegu. “Mavuno kwa ekari moja ni tani nne na kuendelea” alisema Maganga.
Aidha, alishauri kuwa vitunguu vivunwe pale inapoonekana nusu ya mimea shambani imeanza kulegea au kuvunja shingo au kunyauka. “Baada ya kuvuna kata mizizi na majani ya vitunguu kausha kwenye eneo lenye hewa ya kutosha. Hakikisha eneo hilo halina unyevu wala jua kali” alisisitiza Maganga.
Akijibu swali la mkazi wa eneo la Kisasa Jijini hapa, Revina Kongere aliyetaka kujua kwa nini watu wengi hupenda kununua vitunguu vidogo vidogo? Bwana shamba huyo alisema kuwa watu wengi hupenda kununua vitunguu vidogo vidogo kutokana na aina ya familia waliyo nayo. Wengi hawapendi kukata kitunguu na kukibakiza, hupenda kukata na kukitumia chote kwa pishi moja.
Ikumbukwe kuwa zao la kitunguu huhitaji mwinuko wa 0-1900 M kutoka usawa wa bahari na aina ya udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuwamisha maji huku likihitaji kiwango cha mvua 350-550 mm.
Zao la vitunguu likiwa bandani kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati kwenye viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.