MADIWANI wa Halmashauri ya jiji la Dodoma wameshauriwa kukabiliana na athari za lishe duni kwa watoto ili waweze kutoa mchango katika uchumi wa taifa.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alipokuwa akiwasilisha mada juu ya athari za lishe kwa watoto katika mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Juma alisema kuwa lishe duni ina madhara makubwa katika makuzi na mustakabali wa maisha ya mtoto. “Athari za lishe duni kwa watoto zinasababisha madhara ya muda mrefu. Madhara hayo ni udumavu wa kimo na kudhoofika kwa mfumo wa kinga ya mwili ambapo hupelekea kuugua mara kwa mara kwa mtoto” alisema Juma. Athari nyingine ni ukuaji wa ubongo na maendeleo ya mtoto kuwa duni jambo linalosababisha uwezo mdogo wa uzalishaji mali wakati wa umri wa utu uzima.
Athari nyingine alizitaja kuwa ni kiribatumbo kwa watoto. “Waheshimiwa madiwani, kiribatumbo kwa watoto kinachangiwa na uzito uliozidi na kisukari cha mimba kwa mama mjamzito husababisha mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa. Pia kutokuzingatia taratibu sahihi za unyonyeshaji wa maziwa ya mama” alisema Juma. Athari nyingine ni kutozingatia taratibu sahihi za ulishaji wa chakula cha nyongeza kwa watoto na uelewa duni wa wazazi na walezi kuhusu lishe ya watoto.
Afisa lishe alizitaja athari nyingine kuwa ni ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe kwa wingi na mila na desturi zinazoathiri lishe ya watoto zimekuwa ni changamoto kubwa. Maisha ya mtoto kukaa bila kucheza au kufanya mazoezi kwa muda mrefu huathiri hali ya lishe kwa watoto, aliongeza.
Afisa lishe huyo aliwaelezea madiwani mambo ya kuzingatia katika kupanga mlo kamili kuwa ni kutumia vizuri vyakula vinavyopatikana katika mazingira yanayowazunguka. “Mtoto anatakiwa kula angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la vyakula. Kiasi cha chakula hutegemeana na umri, jinsia, shughuli na hali ya kifisiologia ya mtoto” alisema Juma. Vilevile, alisisitiza unywaji wa maji safi na salama na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuufanya mwili kuwa na afya bora.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbabala, Pascazia Mayalla alisema kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo madiwani ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika uhamasishaji masuala ya lishe katika kata zao. “Napenda kuushukuru uongozi wa halmashauri ya jiji kwa kutuandalia mafunzo hayo. Mafunzo haya yamenifundisha kuchanganya chakula vizuri kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula wakati wa kuandaa chakula cha mtoto. Tumekuwa na utaratibu wa kushindilia chakula cha aina moja tu katika mlo wa watoto na sisi wenyewe” alisema Mayalla.
Mayalla alibainisha kuwa wazazi wamekuwa na mchango mkubwa katika udumavu wa watoto. “Watoto tunawaambia mjinga wewe kumbe mzazi ndiye umechangia tatizo hilo. Mama anatakiwa kumuandaa mtoto toka akiwa tumboni kwa mama yake. Udumavu unasababishwa na sisi wazazi si watoto. Wazazi ndiyo tunatakiwa kuwaandaa watoto wetu kwa kuwapa lishe bora” alisisitiza Mayalla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.