Kampuni ya Lonagro imekuja na suluhisho la zana za kilimo kwa lengo la kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara nchini na kuleta tija zaidi.
Kauli hilo imetolewa na Meneja wa tawi la Dodoma, Petro Benjamin alipokuwa akiongelea ushiriki wa kampuni ya Lonagro katika maonesho ya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma.
Benjamin alisema kuwa kampuni yake imekuja na suluhisho la zana za kilimo nchini. “Tumeleta zana kuanzia zinazohusika na uandaaji wa shamba, mpaka uvunaji wa mazao ya wakulima zinapatikana hapa. Tumekuwa karibu na mifumo ya kibenki ambayo wakulima wengi hawafahamu kwamba serikali imeweka fedha za kutosha katika taasisi za kibenki”. Alitolea mfano benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kuwa inawawezesha wakulima kukopa mkopo wa zana kwa kutanguliza kiasi cha asilimia 20 ya jumla ya thamani ya zana zote ambazo mkulima anachukua. “Hivyo, inampa mkulima nafuu ya kulipa mkopo wake kwa miaka mitatu, ambapo kila mwaka mkulima analipa mara moja. Na hivyo, kuchangia kuwainua wakulima wa kawaida” alisema Benjamin.
Kampuni ya Lonagro inajishughulisha na uagizaji na uuzaji wa matrekta aina ya “John Deere” pamoja na vifaa vyote vinavyotumika shambani kwa shughuli za kilimo cha kisasa.
Akiongelea ushiriki wa kampuni yake katika maonesho ya Nanenane, alisema kuwa ni kuwapa wakulima fursa ya kujua zana mbalimbali za kilimo cha kisasa na kufahamu mifumo ya upatikanaji wa matrekta na kuweza kuwaeleza mambo mbalimbali ambayo yanahusu zana mpya zilizo sokoni.
“Tunazo zana mpya kabisa kwa mfano tumewaletea kifaa cha kisasa kabisa ambacho kinaitwa ‘planter’ ambayo inatumiwa kupandia mbegu za mahindi, alizeti na maharage. ‘Planter’ hiyo unaweza kuweka mbegu wakati unapanda na kuweka mbolea moja kwa moja” alisema Benjamin.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma na maeneo mengine kutembelea banda la Lonagro ili kujionea zana mbalimbali za kilimo na jinsi ya kuzipata ili waweze kulima kilimo chenye tija.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.