Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SHULE ya sekondari Lukundo imekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo vinatumiwa na wanafunzi kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Asafu Makonda alipokuwa akisoma taarifa ya shule hiyo kwa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipotembelea na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo.
Mwalimu Makonda alisema kuwa madarasa hayo yamejengwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri. “Katika mwaka wa fedha 2021/2022 tulipokea shilingi 40,000,000 kwa ajili ya kujenga vyumba viwili vya madarasa tarehe 13.10.2021. tumefanikiwa kujenga vyumba viwili ambavyo vimekamilika na vinatumika. Juhudi za ziada za kubana matumizi zilitumika ili fedha hiyo iweze kukamilisha mradi. Aidha, ujenzi huo ulikamilika baada ya kuunganisha vyumba hivi viwili na chumba kilichokuwepo hivyo, kupunguza gharama ya ujenzi wa ukuta wa chumba kimoja” alisema Mwalimu Makonda.
Akiongelea miundombinu ya madarasa katika shule hiyo, alisema kuwa shule ina vyumba vya madarasa 31 sawa na mahitaji ya shule kwa sasa. “Kutokana na kukosekana kwa maktaba, tumeamua kutumia chumba kimoja cha darasa kama maktaba kwa ajili ya walimu na wanafunzi kupata huduma ya maktaba. Samani zilizopo ni meza 1,072 mahitaji 1,316 upungufu 244. Viti vilivyopo 1,079 hamitaji ni 1,316 upungufu ni 307. Mwaka 2020/2021 tunashukuru tulijengewa jengo la utawala, ila halina samani kwa ajili ya walimu. Tunaomba msaada wa meza na viti ili jengo liwe na tija iliyokusudiwa” alisema Mwalimu Makonda.
Ikumbukwe kuwa shule ya sekondari Lukundo ipo katika Kata ya Chang’ombe ikiwa na wanafunzi 1,316 na walimu 45.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.