Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi amewaomba wakazi wa Mtaa wa Mji Mwema, Kata ya Chang’ombe jijini Dodoma kumpatia muda wa miezi mitatu ili atatue mgogoro wa Ardhi uliodumu kwa takribani miaka 40.
Waziri Lukuvi aliyasema hayo leo kwenye mkutano uliofanyika katika Mtaa wa Mji Mwema uliokua na lengo la kumuomba Waziri huyo kusaidia kutatua mgogoro huo ambao umedumu kwa muda mrefu.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Lukuvi aliwataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu kwa kipindi ambacho kamati iliyoundwa itakua ikifanya kazi ya kuhakiki na kumpitia mwananchi mmoja mmoja ili kufanya tathmini na kubaini idadi kamili ya wananchi wenye viwanja katika eneo lenye mgogoro na kuwahakikishia kuwa kila mwananchi atapata haki yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kukubali kuitikia wito huo, na amekua mstari wa mbele katika kutatua migogoro inayojitokeza mkoani hapo.
Dkt. Mahenge alisema kuwa Mkoa kwa kushirikiana na Wizara, pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, TAKUKURU na Vyombo vya Usalama waliunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo, na ilikuja na majibu ambayo wananchi wengi hawakuridhika nayo. Hali hiyo ilipelekea kumuomba Waziri husika aje kusikiliza kero hiyo na kuitatua.
Aidha, akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa iliyokua Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ilitenga eneo hilo lenye Hekta 10 kama sehemu ya makaburi ambapo kwa muda mrefu hakuna shughuli yoyote ya maziko iliyowahi kufanyika katika eneo hilo, jambo ambalo lilipekea zaidi ya wananchi 1,100 kuvamia eneo hilo, na Serikali kuamua kurasimisha sehemu hiyo kuwa makazi ya wananchi mwaka 2014.
Kunambi aliongeza kuwa kiliundwa kikosi kazi ili kuhakiki eneo hilo na taarifa ilibaini zaidi ya wananchi 1,100 kuwepo katika eneo hilo jambo lililoleta mgogoro huo, hivyo kumuomba Waziri Lukuvi kuwasaidia kutatua tatizo hili ili kila mwananchi apatiwe haki yake.
Kwa upande wa wakazi wa eneo hilo wameonesha kuridhishwa na uamuzi wa Waziri Lukuvi na kuwa wako tayari kusubiri kwa hiyo miezi mitatu ili waweze kupatiwa haki yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.