SERIKALI imejipanga kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kushiriki katika uchumi jumuishi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja alipokutana na wanahabari kuzungumzia Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza kuanzia Novemba 21 hadi 26, 2022 yenye kauli mbiu “Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu”.
Dkt. Mwamwaja alisema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masula ya fedha ikiwemo maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili kutimiza lengo la Serikali la kuhakikishasha takriban asilimia 80 ya wananchi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ifikapo mwaka 2025.
“Kutokana na Utafiti wa FinScope wa mwaka 2017 nchini, ni asilimia 48.6 tu ya nguvu kazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza Pato la Taifa”, alifafanua Dkt. Mwamwaja.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imelenga kutumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa, kujenga uchumi na kuondoa umaskini pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha.
Dkt. Mwamwaja alisema wamelenga pia kutoa elimu ya kuwezesha kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha, kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha na kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao.
“Tunalenga kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia elimu ya fedha, kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha, kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni”, alibainisha Dkt. Mwamwaja.
Alisema katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na wadau wengine wa masuala ya fedha zikiwemo wizara, idara, Wakala wa Serikali, wasimamizi wa Sekta ya Fedha, Taasisi za Fedha, Asasi zisizo za kiserikali, Sekta Binafsi, Bodi za Wataalamu, Vyama vya Wafanyakazi, Vyombo vya Habari, Taasisi za Elimu na Utafiti, Washirika wa Maendeleo, Vyama vilele vya Sekta ya Fedha, Makundi ya Watoaji huduma za fedha na Taasisi za Dini zinazotoa huduma hizo.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote hususani wale wanaoishi Kanda ya Ziwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu ili kuweza kupata elimu hiyo muhimu katika kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.