KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI Adolf Ndunguru amewataka maafisa elimu nchini kote kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ujenzi wa miundombinu ya Elimu msingi na sekondari ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Ndunguru ameyasema hayo wakati wa kufunga Mkutano wa kumi wa Maafisa elimu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika katika ukumbi wa Eden jijini Mbeya kwa siku tano ukijumuisha maafisa elimu kutoka mikoa ishirini na sita ya Tanzania bara.
“Nitumie jukwaa hili kusisitiza wito wa serikali kuhakikisha mnasimamia vizuri ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari, hakikisheni kila Halmashauri inakamilisha ujenzi wa miundombinu inayotakiwa’ Ndunguru
Aidha amewataka maafisa elimu hao kuhakikisha waondoa migogoro baina yao ili sekta ya elimu iweze kusonga mbele kwani ni sekta muhimu katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Akihitimisha Mkutano huo ametoa salamu za pole kwa wana Mbeya wote na kutumia nafasi hiyo kufikisha salamu za pole kwa watanzania wote kutokana na madhara yaliyojitokeza ya mafuriko katika baadhi ya meneo nchini Tanzania.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akimkaribisha mgeni rasmi amesema kupitia mkutano huo Ofisi ya Rais TAMISEMI imejiwekea malengo ya kuweza kuboresha utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo na pia kujadili kwa kina kuhusu namna ya kuboresha elimu nchini.
Ameeleza kuwa mkutano huo uliofanyika kwa siku tano ni fursa ya kufanya tathmini katika maeneo yote ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na pili.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu maalum, elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi Bwana Ernest Hinju amesema kikao hicho cha kumi cha Maafisa Elimu Mikoa na Halmashauri kimeibua maazimio 13 ili kuweza kufanya ufuatiliaji wa karibu katika kuhakikisha maendeleo ya elimu nchini yanakwenda kwa kasi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.