Na. Sifa Stanley, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania tawi la Makutupora (Tanzania Agriculture Research Institute- TARI) wametoa mafunzo ya kilimo cha zao la Zabibu kwa maafisa kilimo wa kata za Jiji la Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa agizo la waziri mkuu.
Mafunzo hayo yalitolewa tarehe 4 Agosti, 2021, eneo la Nanenane katika Kata ya Nzuguni, Jijini Dodoma.
Akiongelea mafunzo hayo, Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Agnes Woisso alisema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania tarehe 6 Julai, 2021 alipotembelea na kukagua shughuli katika kituo cha utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Makutupora. Alisema kuwa waziri mkuu aliagiza yatolewe mafunzo ya kilimo cha zao la Zabibu kwa maafisa kilimo wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Katika mafunzo hayo, Mtafiti wa Kilimo kutoka TARI tawi la Makutopora, Dainess Sanga alielezea namna nzuri ya kuandaa shamba la zabibu, uchaguzi mzuri wa mbegu, uandaaji wa mbegu, pamoja na uandaaji wa mbolea na matumizi sahihi ya mbolea. Vilevile, alielezea aina mbalimbali ya Zabibu pamoja na matumizi yake. “Ni muhimu kuzingatia aina bora ya mbegu na kufanya maandalizi mazuri ya upandaji wa mbegu ili kupata mavuno mazuri” alisema Sanga.
Kwa upande mwingine Prosper Rema, ambaye ni afisa kilimo kutoka TARI tawi la Makutupora alitoa mafunzo ya namna bora ya ukataji wa mbegu za Zabibu na dawa bora za zao hilo Pamoja na njia bora ya upigaji dawa wa zao la Zabibu. Aidha, aliwafundisha maafisa kilimo wa halmashauri jinsi ya kuhudumia mmea wa zao la Zabibu ambapo mafunzo hayo aliyafanya kwa vitendo katika vitaru vya zao la Zabibu.
“Huduma nzuri ya mmea huchangia ukuaji mzuri wa mmea na mazao huwa ya kuridhisha. Hivyo, ni vema kuzingatia huduma kwa mmea” alieleza Rema.
Akiongelea umuhimu wa mafunzo hayo, Afisa Kilimo kutoka Kata ya Ihumwa, Swaiba Msangi alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa ujuzi wa njia bora ya kulima zao la Zabibu. “Mafunzo haya yamenisaidia kupata ujuzi wa namna bora ya kufanya kilimo cha zao la Zabibu. Mafunzo haya yataimarisha kilimo hicho katika Jiji la Dodoma” alisema Msangi.
Aidha, ameiomba serikali kuimarisha masoko ya zao la Zabibu kwa kuhamasisha wawekezaji zaidi kununua zao hilo kutokana na soko la ndani na nje ya nchi kuwa changamoto.
Mafunzo hayo endelevu yalihudhuriwa na Maafisa kilimo kumi na saba wa ngazi za kata, watafiti wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa kilimo, tawi la Makutupora.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.