Na Sifa Stanley, DODOMA
MAAFISA kilimo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamepatiwa mafunzo endelevu ya kilimo cha zao la zabibu ili kulipa thamani na kuongeza mavuno ya zao hilo lililotangazwa na serikali kuwa la kimkakati hivi karibuni.
Mafunzo hayo yalifanyika katika shamba la zabibu lililopo eneo la Hombolo, ambayo ni endelevu na ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu aliyeagiza Maafisa kilimo wapatiwe mafunzo ili kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa zao la kimkakati na lenye tija katika Taifa.
Akielezea manufaa ya mafunzo hayo, Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Agness Woisso alisema kuwa mafunzo yanayoendelea kutolewa yatasaidia kuongeza mavuno na ubora wa zao hilo. Halmashauri imejipanga kuandaa miche laki tano ambayo wataigawa kwa wakulima wa zabibu, aliongeza.
“Sisi tumejipanga kuandaa miche laki tano ambayo mbegu zake zinapatikana katika maeneo ya Gawaye, Hombolo na Matumbulu. Tunachukua mbegu hizo tunapeleka Nanenane ambapo miche inazalishwa pale. Tunazalisha mbegu hizo kisha tutagawa mbegu kwa wakulima wakati wa msimu wa kilimo cha Zabibu” alifafanua zaidi Woisso.
Kwa upande wake mtaalamu wa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, William Luhamba alitoa wito kwa wakulima wa zabibu jijini hapo kutambua thamani ya zao hilo. Pia alisisitiza wafuate maelekezo ya wataalamu ili kuweza kufanya uzalishaji mkubwa wa zao hilo.
“Japo Halmashauri imejipanga kuandaa miche kwa ajili yao, na wao wakulima wanapaswa kuandaa mashamba yao kwa kupanda mbegu mpya na kuondoa mbegu za zamani. Pia wakulima watambue thamani ya zao hili na kulipa kipaumbele ili liongeze pato la taifa” alisema Luhamba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.