Serikali imewataka Maafisa Mawasiliano, Habari na Uhusiano kutumia ujuzi na weledi wao kuisemea, kuitangaza mipango na mikakati ya Serikali kwa haraka, ukweli na uhakika kimkakati ili ujumbe huo uwafikie walengwa kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa Wasemaji wa Serikali toka Wizara, Taasisi za Serikali, Wakala mbalimbali za Serikali, Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo.
“kwa mafunzo haya mliyoyapata, ninyi mkiwa kama Wasemaji wa Serikali katika maeneo yenu ya kazi, mtaweza kuhabarisha wananchi kuhusu miradi na utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali”. Alisema Mhandisi Nyamhanga.
Amesema ni muhimu sasa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara na endelevu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika kuhabarisha Umma masuala ya kimaendeleo na kiuchumi kwa jamii
“ni muhimu sana kuwa na mafunzo ya mara kwa mara ambayo yanawaongezeeni ujuzi ili muweze kwenda na wakati katika kufikisha habari kwa walengwa, mwendelezo wa kujinoa katika kufikisha habari na taarifa sahihi kwa wakati”
Aidha, amesema Mafunzo ya mawasiliano ya kimkakati ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo Serikali ya Awamu ya Tano inafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kama vile Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme (Julius Nyerere Hydro-Power Project) wa Megawati 2115, Ujenzi wa vituo vya afya 352, hospitali za wilaya 67 na 27 katika mwaka 2019/2020 na zahanati, miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, na utoaji wa Elimu Bila Malipo ambao kwa 2019/2020 shilingi 288.485 zimetengwa.
Mageuzi mengine ni pamoja na sheria mpya ya mapato ambapo mapato ya madini pekee yanatarajiwa kufikia shilingi Bilioni 420 mwaka 2019/2020, ununuzi wa ndege mpya na ujenzi wa treni ya umeme ya kisasa (Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaam – Morogoro shilingi trilioni saba.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Jonas Kamaleki amesema mafunzo hayo ya siku tano yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa hao ili waweze kutoa taarifa kwa usahihi, umakini na wakati, kutoa taarifa kimkakati, kutoa taarifa kwa Umma kwa mpangilio wa kisasa, usahihi na weledi.
Naye Bi. Sarah Kibonde Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) amesema katika mafunzo hayo jumla ya washiriki 141 wamehudhuria na yamelenga zaidi kuwajengea uwezo Maafisa hao ili wawee kufanya kazi zao kwa weledi.
Akiongea kwa niaba ya washiriki, Benton Nollo Afisa Habari kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma amesema ofisi za Maafisa hao hasa katika Mikoa na Halmashauri nchini wanakabiliwa na uhaba wa vifaa, bajeti ndogo, kutotakumbulika kwa Vitengo vya Habari na kutoshirikishwa kwenye baadhi ya miradi ya Maendeleo kwenye maeneo yao.
Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa chini ya Idara ya Habari Maelezo na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) ambapo Maafisa na Wasemaji hao walijifunza kuhusu uandikaji wa habari kwa weledi, taarifa kwa Umma (Press Release), kuandaa vipindi bora vya televisheni na utumiaji wa mitandao ya kijamii.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.