Katika kutekeleza agizo la Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan, juu ya kutunza mazingira, wataalam wa mazingira kutoka jiji la Dodoma kwa kushirikiana na viongozi wa kata ya Ntyuka, leo wamefanya operesheni ya kukagua stakabadhi za malipo ya vifusi vya mchanga kwenye vifanda vya tofali vilivyopo kata hiyo ili kubaini watu wanaochimba mchanga na kusafirisha usiku katika eneo la mtaa wa Chidachi lililozuiliwa kwa mujibu wa sheria za mazingira.
Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu Jiji la Dodoma Dickson Kimaro amesema, kutokana na baadhi ya watu wanaomiliki viwanda kula njama na wamiliki wa malori kusafirisha mchanga na kuumwaga nyakati za usiku, opereshani hizi zitafanyika mara kwa mara kwa lengo la kukagua stakabadhi za ununuzi wa mchanga kutoka kwa wamiliki wa malori ya kubebea mchanga.
Kimaro ameagiza wafanyabiashara wote wenye viwanda vya tofari na wananchi wanaofanya ujenzi wahakikishe wanachimba mchanga maeneo yaliyoruhusiwa ambayo ni Zuzu, Mtumba, Ihumwa, Iyumbu na Mpunguzi. Watu wote wahakikishe wanapatiwa stakabadhi halali, la sivyo watatafsiriwa kuwa wezi na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani.
Diwani wa kata ya Ntyuka Mheshimiwa Teobart Maina amesema zaidi ya hekta 20 zimeharibiwa vibaya na wachimbaji wa mchanga likiwemo eneo la Ukanda wa Kijani. Kwa kutambua umuhimu wa eneo hilo Maina amesema doria za mara kwa mara zitaendelea kufanyika ili kuwadhibiti wezi wa madini ujenzi hasa nyakati za usiku.
Afisa Mtendaji wa kata ya Ntyuka Vestina Manota amewaagiza wamiliki wa viwanda vya tofali kuhakikisha wanachukua taarifa za watu wanaowauzia mchanga kwa kuandika jina la dereva, namba ya simu, namba ya gari linalobeba mchanga na nakala ya stakabadhi za malipo ya ushuru.
Naye Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Chidachi Merina Nzunda amesema wataendelea kufanya doria katika eneo hilo kila siku na kupita katika viwanda vya tofari ili kukagua stakabadhi na taarifa zote zitapelekwa kwa Mtendaji wa kata.
Jitihada hizi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zina lengo la kuhakikisha kasi ya ujenzi katika jiji la Dodoma inaenda sambamba na utunzaji wa mazingira.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.