Na. Shaban Ally, DODOMA.
NAIBU MEYA wa Jiji la Dodoma, Mhe. Emmanuel Chibago ameongoza zoezi la kukabidhi pikipiki kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri ya jiji la Dodoma ili kuboresha huduma ya kilimo kwa wakulima ndani ya halmashauri hiyo.
Zoezi hilo limefanyika kwenye ofisi za Idara ya Kilimo ambapo Chibago alikabidhi takribani pikipiki 25 kwa maafisa Ugani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ili kuongeza ufanisi kwenye majukumu yao lakini pia Chibago hakusita kutoa pongezi kwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia maafisa Kilimo pikipiki ili kurahisisha utendaji wao wa kazi. Aidha makabidhiano hayo yamefanyika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu alilolitoa kwa Wizara ya Kilimo kuhakikisha pikipiki hizo ziwafafikia walengwa katika kipindi cha siku tano kuanzia leo tarehe 8 Juni, 2022.
"Tunaomba tutoe pongezi kubwa kwa Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan kwa hiki alichokifanya kwa kutoa vyombo hivi vya usafiri kwa maafisa wetu wa Kilimo, kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kugawa vitendea kazi kwa maafisa ugani tuliowaamini kufanya kazi hii, kinafungua ukurasa mpya wa muendelezo wa Kilimo chetu”, alisema Chibago.
Kwa upande mwingine Mkuu wa idara ya Kilimo, Yustina Munishi akielezea malengo ya Wizara ya Kilimo mpaka kufikia mwaka 2030, alisema "Tunakabidhi pikipiki takribani 25 kwa lengo la kutekeleza ajenda ya kilimo kufikia 2030 mchango wa Kilimo kwenye uchumi wa nchi uongezeke kwa 10%".
Yustina aliongeza kuwa maafisa Kilimo wamepewa pikipiki hizo kwa lengo la kuwezesha kutekeleza ajenda zilizowekwa na wizara ya kilimo ambapo ni kutoa huduma bora za ugani, kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao pamoja na kutoa elimu bora kwa wakulima.
Sambamba na hilo, Chibago aliwaasa maafisa ugani waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitumia kwa shughuli za Kilimo tu na si vinginevyo, "Kupitia makabidhiano haya niwaase ndugu zetu maafisa ugani ambao mmekabidhiwa vifaa hivi kuwa vitumike kwa kuhudumia wakulima na si kubebea mkaa".
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.