UJUMBE wa Maafisa wa Serikali ya Nigeria wapatao 33 umeanza ziara ya siku Nane nchini kujifunza namna Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF unavyotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini-PSSN.
Akiwakaribisha Maafisa hao, Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF, Bwana Amadeus Kamagenge amesema Mkakati wa Serikali ya Tanzania kupambana na umaskini kupitia TASAF umekuwa na mafanikio makubwa na umeamsha ari ya wananchi kuboresha maisha yao.
Bwana Kamagenge amesema mkazo mkubwa umewekwa katika uhamasishaji wa Walengwa kushiriki kwenye kazi za uzalishaji mali huku sekta ya elimu na afya hususani kwa watoto kutoka katika kaya za Walengwa zikipewa msukumo mkubwa zaidi kwenye shughuli za Mpango.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Miradi wa TASAF amesema mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa shughuli za Mpango yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na ushiriki wa Walengwa na Mchango mkubwa wa Serikali na Wadau mbalimbali wa Maendeleo.
Kwa upande wao Maafisa hao kutoka nchini Nigeria wamesema uamuzi wa kuja Tanzania kujifunza umetokana na taarifa walizonazo juu ya mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Tanzania kupitia TASAF imepata kwa kuzifikia Kaya za Walengwa na kuzihudumia kwa mafanikio makubwa katika kupunguza kero ya umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao ni wa aina yake kupata kutekelezwa barani Afrika.
Ujumbe huo wa Maafisa kutoka Nigeria, mbali na kupata maelezo ya shughuli za TASAF katika Ofisi ndogo za Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam pia utapata fursa ya kutembelea Unguja ambako utakutana na Maafisa wa Serikali na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kisiwani humo. Hii ni mara ya Pili kwa Maafisa wa serikali kutoka Nigeria kutembelea Tanzania kujifunza namna TASAF inavyotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Chanzo: Blog ya TASAF
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.