Na. Faraja Mbise, DODOMA
Maafisa waandikishaji orodha ya wapiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuwa waadilifu ili Dodoma iwe ya Kwanza kwa idadi kubwa ya watu walioandikishwa.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dodoma, ColethaKiwale wakati akizungumza na maafisa waandikishaji, watendaji wa mitaa, wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata pamoja na maafisa watendaji wa kata wakati wa mafunzo kwa maafisa waandikishaji wa orodha ya wapiga kura leo katika ukumbi wa Mtumba Complex jijini Dodoma.
Kiwale aliwataka maafisa waandikishaji kuwa weledi na wenye ufanisi katika suala la muda, mavazi na utoaji taarifa kwa wakati. Msisitizo mwingine alisisitiza wawe waadilifu na wahamasishaji kwa waandikishaji kujitokeza
kwa wingi katika kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura.
“Napenda tushirikishane tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tungependa kuwaambia mambo ya kuzingatia mambo yafuatayo: moja, muda wa kufungua vituo na kufunga vituo. Pili, Tunawaomba maafisa
uandikishaji kuwa wahamasishaji wa watu kuja kujiandikisha, pamoja na familia zao kwasababu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma anatamani Dodoma iongoze kwa idadi kubwa ya watu watakaokuwa wamejiandikisha kwenye orodha ya daftari nchi nzima, kutoa taarifa za uandikishaji mpaka inapofika saa moja na nusu jioni kwa kufuata muundo wa kitaasisi. Maafisa waandikishaji kuripoti kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa. Pia hatutarajii Afisa Mwandikishaji kutafutwa kwenye simu na asipatikane” alisisitiza Kiwale.
Kwa upande wake CPA. Eric Ntikahera, aliwataka maafisa waandikishaji kufanya mambo muhimu tu yanayohusu zoezi la uandikishaji. Aliwataka wafuate maadili na kanuni za utumishi na uadilifu pindi wawapo katika vituo vya
kujiandikisha. Vilevile, aliwataka wasigeuze vituo hivyo kama sehemu ya starehe bali waheshimu vituo hivyo vya kuandikishia kama wanavyoheshimu sehemu nyingine za kazi.
“Mwaka 2019 tulifundisha maafisa waandikishaji wakaelewa, lakini nafikiri ilikuwa vitu viwili tofauti, mtu kapewa elfu kumi yake ya chakula yeye kanunua bia nne pembeni, yaani uandikishaji unaendelea na ulevi
unaendelea. Kwahiyo, kimsingi tijiepushe katika vitu vitakavyokwamisha hili zoezi” alisema CPA. Ntikahera.
Wakati huohuo, Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga alipokea salamu hizo kutoka Ofisiya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kuahidi utekelezaji katika zoezi la uandikishaji orodha wa wapiga kura kwa
weledi. “Tunamuahidi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutekeleza yale aliyoagiza ili Dodoma iwe ya kwanza katika zoezi la uandikishaji kwenye orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchi nzima” alisema Kasoga.
Ikumbukwe kuwa zoezi hilo la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura halitahusisha uwepo wa kadi au kitambulisho cha mpiga kura, ilimradi tu mwananchi awe amejiandikisha katika orodha ya wapiga kura, vitambulisho vitakavyohusika ni leseni ya udereva, kadi ya Bima ya Afya, kitambulisho cha kazi au kitambulisho cha Taifa (NIDA). Iwapo mwananchi hana atatambulishwa na jirani yake wa mtaa husika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.