Na: Hellen M. Minja
Habari - DODOMA RS
Maambukizi ya Ugonjwa wa Homa ya Ini aina ‘B’ yafikia kiwango cha 3.5% kulingana na utafiti wa Kitaifa uliofanywa mwaka 2022. Hayo yamebainishwa na Meneja Mapango wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Dr. Prosper Faustine Njau wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jijini humu.
Mkutano huo umefanyika ukilenga kuutangazia Umma juu ya Maadhimisho ya siku ya Homa ya Ini Duniani ambayo hufanyika Julai 28 ya kila mwaka, na mwaka huu Kitaifa yanatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Morena Jijini Dodoma yakihudhuriwa na Mgeni rasmi Waziri mwenye dhamana ya Afya Mhe. Jenista Mhagama (MB).
“Kulingana na utafiti wa Kitaifa uliofanywa mwaka 2022, ushamiri wa maambukizi ya Homa ya Ini ni ya aina ‘B’ ni 3.5% kwa watu wenye umri kuanzia miaka 15 mpaka 60. Tunaweza kuona ni tatizo kubwa kwa sababu kama ilivyo maambukizi ya Ukimwi Kitaifa ni 4.5% tunaweza kuona hapa Homa ya Ini inakaribia hapo”. Dr. Njau.
Aidha, ameongeza kuwa, Kitaifa wanalenga homa ya Ini aina mbili ambazo ni ‘B’ na ‘C’ambapo homa ya Ini aina C’ ushamiri wake ni 0.2% Kitaifa hali inayoonesha kuwa maambukizi yake ni madogo ingawa ni hatari na aina hii imekua ikiwaathiri zaidi wale wanaotumia Dawa za kulevya.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dr. Nelson Bukuru amesema maadhimisho hayo kwa Mkoa yataanza Julai 26 hadi siku ya kilele Julai 28 ambapo shughuli mbalimbali za utoaji wa Huduma za upimaji afya zitafanyika katika viwanja vya zamani vya Mashujaa vilivyopo Jamatini Jijini humu.
Hata hivyo, ametaja huduma za afya zitakazotolewa katika kipindi hicho kuwa ni utoaji wa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Ini, chanjo, upimaji na matibabu kwa wale watakaogundulika na tatizo hilo sambamba na kupatiwa rufaa itakapobidi ambapo huduma zote hizo zitatolewa bila gharama yoyote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.