Na. Dennis Gondwe na Theresia Nkwanga, DODOMA
AFYA bora ni nguzo muhimu sana Katika kuhakikisha wananchi wana ukamilifu wa mwili, akili na kuepuka maradhi.Katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya.
Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua katika kuboresha huduma za Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiongeza vituo vya kutoa huduma za Afya kufikia 116.
Maendeleo ya taifa ni mchakato unaoanzia katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia, jamii hadi ngazi ya taifa. Ili dhana ya maendeleo iwe halisia na yenye maana suala la wananchi kuwa na afya njema haliwezi kupingika. Katika kuamini kwenye dhana hiyo miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita imejielekeza katika kuboresha sekta ya afya ili wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Makao Makuu ya nchi wawe na afya bora.
Mkuu wa Divisheni ya Afya, Utawi wa Jamii na Lishe katikaHalmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method anasema katika miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan vituo vya kutolea huduma za Afya vimeongezeka kutoka vituo 100 mwaka 2020 hadi kufikia vituo 116 mwaka 2023. Kati ya vituo hivyo,Hospitali zipo saba, kati ya hizo hospitali mbili ni za serikali, Mashirika ya dini hospitali mbili,Mashirika ya Umma hospitali mbili, na watu binafsi Hospitali moja. Vituo vya Afya ni 12, kati ya hivyo, vituo vitano ni vya serikali, kimoja ni cha shirika la dini, vituo vitatu ni vya mashirika ya umma na vituo vitatu ni vya watu binafsi.
Ongezeko hilo linatajwa pia katika Zahanati. Zahanati zipo 81 ambazo zimegawanyika kama ifuatavyo; zahanati za serikali 37, mashirika ya dini 11,mashirika ya umma tisa, zahanati zawatu binafisi 24. Kuna jumla ya kliniki maalumu 14 zinazomilikiwa na watu binafsi. Kituo cha uchunguzi kimoja(Diagnostic center) na maternity home moja anasema Dkt. Method.
Ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya limeenda sambamba na ongezeko la watumishi wa sekta ya Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita watumishi wameongezeka kutoka watumishi 472 hadi kufikia watumishi 509.
Ongezeko hilo linatokana na Halmashauri kupata watumishi wapya 37 wa sekta ya Afya sawa na ongezeko la asilimia nne ya watumishi wanaohitajika. Watumishi hao wamepangwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Ama kwa hakika hakuna kama Mama, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa kipaumbele kwenye huduma za afya kwa kuboresha huduma na kuhakikisha zinawafikia wananchi wote alisisitiza Daktari Andrew
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.