HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yakamilisha ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana katika shule ya sekondari Dodoma kwa shilingi 275,000,000 katika mwaka wa fedha 2018/2019
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Kunambi alisema “kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana Shule ya Sekondari Dodoma kwa thamani ya shilingi 275,000,000 ambapo shilingi 120,000,000 kutoka fedha za mapato ya ndani na shilingi 155,000,000 fedha toka serikali kuu”. Katika mwaka huo wa fedha, Halmashauri ilifanikiwa kununua vitanda 63 vyenye thamani ya shilingi 19,900,000 kwa shule za sekondari Dodoma na Hombolo.
Jumla ya vyumba 90 vya madarasa vilijengwa. Kati ya vyumba hivyo, vyumba 38 ni katika shule za msingi na vyumba 52 katika shule za sekondari. Alisema kuwa ujenzi huo wa madarasa ni ongezeko la vyumba 31 vya madarasa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2017/2018 vilipojengwa vyumba 59 vya madarasa. Shule za sekondari vilikuwa vyumba 14 na shule za msingi vilijengwa vyumba 45.
Akiongelea ujenzi wa nyumba za walimu kwa mwaka wa fedha 2018/2019, alisema kuwa nyumba nane za walimu zilijengwa. Katika nyumba hizo nyumba nne zilikuwa kwa ajili ya shule za msingi na nyumba nne nyingine za shule za sekondari. Ujenzi wa nyumba hizo ni ongezeko la nyumba sita ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2017/2018 zilipojengwa nyumba mbili za walimu. Nyumba moja kwa shule ya msingi na nyingine kwa shule ya sekondari.
Kwa upande wa ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi, alisema kuwa maabara nane zaidi zimejengwa na kukamilishwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2017/2018. “Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Maabara za shule ya sekondari zilizokamilika zipo 16 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2017/2018 zilikuwa maabara 8” alisema Kunambi.
Halmashauri ilitengeneza madawati 1,000 mwaka wa fedha 2018/2019 kwa kutumia mapato ya ndani ikilinganishwa na mwa wa fedha 2017/2018 yalipotengenezwa madawati 163 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 83.7.
Maboresho ya miundombinu katika sekta ya elimu yamesaidia kuongeza ufaulu katika halmashauri, alisema mkurugenzi. Mwaka wa fedha 2018/2019 shule ya msingi wanafunzi waliofaulu darasa la saba walikuwa 80,838 kati ya wanafunzi 10,103 waliofanya mtihani sawa na asilimia 79.56. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 wanafunzi 6,488 walifaulu kati ya wanafunzi 9,509 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi sawa na asilimia 68.
“Ufaulu wa wanafunzi kwa shule za sekondari mwaka wa fedha 2018/2019 kidato cha nne wanafunzi waliofanya mtihani na kufaulu walikuwa 3,472 Kati ya wanafunzi 4,541 waliofanya mtihani sawa na asilimia 76.05 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2017/2018, wanafunzi waliofanya mtihani na kufaulu walikuwa 3,080 kati ya wanafunzi 4174 waliofanya mtihani sawa na asilimia 74.05” alisema Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.