Na Getruda Shomi, DODOMA
MACHIFU wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Chifu Mkuu wa Kanda ya Kati Mazengo II, wamemkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.
Wametoa tamko la kumkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya katika hafla iliyofanyika leo Agosti 6, 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo walikutana na Mkuu huyo wa Wilaya.
Akiongoza hafla hiyo, Chifu Mazengo II alimkabidhi Mhe. Shekimweri kiti cha miguu mitatu na shuka ikiwa ni ishara ya upendo, amani na ushirikiano.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Dodoma alipewa jina la Bilinje na Machifu hao ikiwa ni kumkaribisha na kumpa utawala wa Kichifu katika Wilaya ya Dodoma na kuwa ni mshauri wa Baraza la Machifu.
“Sisi ni Wagogo na wewe tunakukaribisha katika Ugogo, kwa maana hiyo tunakuomba uwe mshauri katika Baraza la Machifu”.
Hata hivyo, risala ya Machifu hao iliyosomwa na Katibu Msaidizi wa Machifu, Chifu Ally Issa Bilinje wa Dodoma Makulu ndugu Jackson Ligoha iliezea changamoto za Machifu ikiwemo, kukosa ofisi, usafiri, semina kwa Machifu, lakini pia risala hiyo ilimuomba Mkuu huyo wa Wilaya kuanzisha sehemu ya Makumbusho kwa ajili ya utalii ikiwemo Maliteli, uhunzi na Ufinyanzi ili kuhamasisha watu kujifunza historia ya Jiji la Dodoma.
Katika hafla hiyo Chifu Mazengo II aliainisha kazi zinazofanywa na Machifu hao kuwa ni pamoja na kuhimiza maendeleo ya nchi, kukemea mambo maovu yanayotendeka katika jamii, na kurudisha mahusiano mema katika sehemu zisizo na maelewano.
Aidha, aliwaomba Machifu wenzake wawe mabalozi katika jamii zao kuhimiza watu kupata chanjo ya UVIKO-19 inayotolewa katika vituo vya afya elekezi Jijini humo.
”Ndugu Machifu na wajumbe wote mliofika, sasa hivi tuna gonjwa hili la Corona, tunamshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameliona hilo na ametuletea chanjo, basi sisi tuwe mabalozi, tuhamasishe watu wajitokeze kwa ajili ya chanjo” alisema.
Aliongeza kuwa gonjwa hilo linaua hivyo kila Chief ahimize wakazi wa eneo lake kupata chanjo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.