HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepanga kuwahamisha wafanyabiashara wadogo walioenea katika mitaa mbalimbali ya Jiji hilo na kuwapeleka kwenye eneo la wazi la ‘Bahi road’ ili wafanye biashara zao katika eneo hilo linalofikika kirahisi na lenye mzunguko mkubwa wa watu.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru aliliambia Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kuwa, baada ya maelekezo ya Serikali kuhusu kuwapanga kwa utaratibu mzuri wafanyabiashara hao, Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa na Chuo cha Ardhi walikagua maeneo saba tofauti ili kupata eneo zuri zaidi la wafanyabiashara hao kuhamia kwa ajili ya shughuli zao.
Mafuru alikuwa akijibu swali la papo kwa papo la diwani wa Kata ya Nkuhungu Mhe. Daudi Mkhandi aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ya Jiji kuhusu suala kuwapanga wamachinga baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa agizo la kupangwa vizuri kwa wafanyabiashara hao bila kuathiri shughuli zao.
Mkurugenzi Mafuru alisema eneo la 'Bahi road' ni muafaka kwa wafanyabiashara hao na kwamba walishafanya nao kikao na kwamba Halmashauri itaweka sakafu ya mawe katika eneo hilo na kujenga vibanda vidogo ambavyo vitatumiwa kuwekea bidhaa za wafanyabiashara hao.
“Mheshimiwa mwenyekiti, baada ya agizo la Mhe. Rais sisi hatukutaka kuwaswaga tu wamachinga bali tunataka kuwaboreshea mazingira ya kazi zao kwa kuwaandalia eneo zuri sana pale 'Bahi road', eneo lile lina uwezo wa kuchukua zaidi ya machinga 2,000 na sisi jiji la Dodoma tuna takribani machinga 1950” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Alisema Jiji limekuja na mpango wa kushirikiana na wataalam wa Chuo cha Ardhi ili watengeneze mazingira ya kisasa ya eneo la kibiashara ili pia kuupendezesha mji na kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara hao na tayari kazi imeshaanza.
Diwani wa Kata ya Nkuhungu Mhe. Daudi Mkhandi.
Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Baadhi ya waalikwa wa Mkutano wa Baraza la Madiwani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.