HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imesaini mkataba na kampuni ya Mohamed Builders Limited wa ujenzi wa awamu ya kwanza Jengo la kisasa la wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga Open Market) kwa thamani ya shilingi Bilioni 4.95 kwa ujenzi wa awamu ya kwanza, ambapo hadi kukamilika mradi huo utagharimu shilingi bilioni 7.5 fedha kutoka katika mapato ya ndani na zingine kutoka serikali kuu
Mradi huo unatekelezwa eneo la Bahi Road Jijini humo na utachukua eneo la mita za mraba 14,235 ambapo ujenzi wa mradi kwa awamu ya kwanza utatekelezwa kwa muda wa miezi minne yaani siku 120.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema kujengwa kwa mradi huo kutakuwa na faida nyingi kwa wafanya biashara na Taifa kwa ujumla ikiwemo ukusanyaji wa mapato, kuliweka jiji la Dodoma katika mandhari safi, pamoja na kurahisisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira.
Mafuru alisema wafanyabiashara ndogo wapatao 2,938 watakuwa na ajira ya uhakika kwa kufanya biashara katika eneo maalum linalotambulika na kurahisisha utoaji wa huduma za msingi kwa wafanyabiashara hao kama huduma za vyoo, huduma za kifedha, na ulinzi wa mali zao.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kujengwa kwa mradi huu kutakuwa na faida nyingi kwa Jiji la Dodoma, wafanyabiashara, na Taifa kwa ujumla hapa naelezea baadhi ya faida hizo kuwa ni Pamoja na ukusanyaji wa mapato, kuliweka Jiji la Dodoma katika mandhari safi, kurahisisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira” alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa, Anthony Mtaka akiwa mgeni rasmi katika tukio hilo alisema kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni ukombozi na hatua kubwa kwa wafanyabiashara hao ambapo watahamia kwa hiari yao katika eneo hilo na kutoka katika maeneo yasiyo tambulika kisheria.
Mkuu huyo wa Mkoa alikemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara ndogo kujisajili kwa majina ya udanganyifu huku ikiwa ni mbinu ya kuwasajilia watu wasio walengwa katika mradi ambapo alisema watakaobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Mkurugenzi tukishakamilisha ujenzi wa eneo hili hatutarajii kuona kuna Machinga yeyote atakayeshindwa kuhamia katika eneo linalotambulika kisheria, matarajio yangu ni kwamba viongozi wa wafanyabiashara hawa watatusaidia katika kusimamia hilo” alisema.
“Naomba kukemea baadhi ya tabia zilizoibuka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kujiorodhesha kwa majina ya udanganyifu kwa lengo la kuwashikia maeneo watu wasio walengwa wa mradi huu, tukikubaini katika vitendo hivyo hautaruhusiwa kufanya biashara katika eneo hili, tutakutoa mara moja ” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Mtaka.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo Bruno Mponzi alisema wafanyabiashara hao wamepata matumaini makubwa ya kukua kibiashara kwa kupata eneo hilo kwani kutasaidia wao kukuza mitaji na kukatatua kero walizokuwa wakikutana nazo katika maeneo yasiyo rasmi .
“Viongozi wakuu wote, kwa niaba ya machinga wote tunaona faraja na tunajivunia uongozi wenu, kwani kwa eneo hili lenye ukubwa wa kutosha tuna matumaini sasa tunakwenda kukuza mitaji yetu na uwepo wa eneo hili sasa unatatua ile changamoto na adha tulizokuwa tunakutanana nazo katika maeneo yasiyo rasimi” alisema Mponzi.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mohamed Builders Limited, Taher Mustafa alisema watatekeleza mradi kwa muda sahihi kwa mujibu wa mkataba ambao ni miezi minne.
“Kampuni yetu ya Mohamed Builders Limited imetekeleza miradi mingi ya Serikali hivyo tunashukuru kwa kupata tena nafasi nyingine ya kutekeleza mradi huu, sisi kama kampuni tutajitahidi kukamilisha mradi huu ndani ya muda husika kama ilivyo katika makubaliano ya mkataba wetu” alisema Mustafa.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka aliyekuwa mgeni rasmi wa utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa eneo maalum la wafanyabiashara wadogo 'Machinga' Jijini Dodoma katika eneo la Bahi Road.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru.
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wadogo 'machinga' waliohudhuria utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa eneo la machinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mohamed Builders Limited, Taher Mustafa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.