WAFANYABIASHARA wadogo maarufu kama Machinga katika Manispaa ya Dodoma wanatarajiwa kupewa eneo lililotengwa rasmi na Halmashauri ya Manispaa hiyo kwa ajili ya biashara zao lililopo katika Kata ya Makole mjini humo.
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma chini ya Mkurugenzi Godwin Kunambi imekamilisha uwekaji wa miundombinu muhimu katika eneo hilo maarufu kama ‘Makole D-Center’ ikiwemo choo, ambapo wakati wowote wafanyabiashara hao watahamishiwa kwa utaratibu utakaoratibiwa na Manispaa kwa kushirikiana na uongozi wa wafanyabiashara hao.
Katika hatua za awali za maandalizi ya eneo hilo, Halmashauri pamoja na mambo mengine, iliondoa makazi ya Bibi Elizabeth Sonyo aliyekuwa akiishi katika eneo hilo kinyume cha Sheria.
Hata hivyo, kutokana na Bibi huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 75 kutokuwa na uwezo wa kujenga, Manispaa ilibeba jukumu la kumjengea makazi mapya na bora zaidi katika eneo jingine, ambapo amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kitendo hicho kwani hakuwa na uhalali wa kisheria wa kuishi katika hilo na kwamba angeweza kuondolewa bila kupewa msaada wowote.
Kwa mujibu wa Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Ludigija Ndwata, kazi iliyobaki ni kuweka mawe maalum (gravels) katika eneo hilo ili livutie zaidi na liwe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja, kabla ya matumizi kuanza.
Halmashauri ya Manispaa pia inaandaa eneo la ‘Chaduru D-center’ kwa ajili ya kulirasimisha kwa matumizi ya wafanyabiashara wadogo hususan akina mama wanaouza vyakula, mbogamboga, na matunda.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.