Halmashauri ya Jiji la Dodmoa, imetoa onyo kwa wafanyabiashara wadogo (Machinga) kuacha kupanga bidhaa zao kabla ya muda uliopangwa kwenye barabara pembeni ya Nyerere Square inayotumika kama 'soko la jioni' ili kutozuia watumiaji wengine wa barabara.
Katika barabara hiyo, wafanyabiashara hao wanapaswa kupanga bidhaa zao kuanzia saa 10:00 jioni baada ya muda wa kazi kuisha, lakini wameonekana kukiuka utaratibu huo na kuanza kupanga kabla ya muda huo.
Onyo hilo lilitolewa jana na Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara hao wanaofanya biashara katika eneo hilo.
Alisema hivi sasa wamekuwa wakipanga bidhaa muda wa asubuhi hali inayoleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Wafanyabiashara mnapaswa kufuata sheria, kanuni na maagizo yaliyoelekezwa na jiji ya kufanya biashara zao kwa muda waliopangiwa ili barabara hii itumike kwa shughuli nyingine,” alisema.
Aliongeza: “Jiji halitakuwa tayari kuwaona baadhi yenu mkikiuka maelekezo mliyopewa ya kufanya biashara zenu kwa muda mlioambiwa wa kuanzia saa kumi hadi saa tatu usiku, vinginevyo tutawaondoa bila nyinyi kupenda suala ambalo halina tija kwa pande zote hivyo ninawataka mzingatie maelekezo na si vinginevyo.”
Sambamba na hilo, aliwataka kuzingatia usafi kwenye maeneo ambayo wamekuwa wakifanya biashara zao.
“Hii ni pamoja na kutokiuka maelekezo ya maeneo mnayotakiwa kufanya shughuli zenu ili kuepukana kuondolewa kwa nguvu na kusababisha hasara ya bidhaa zenu,” alisema.
Kadhalika, ofisa huyo alisema kuwa bado kuna tatizo kwa baadhi ya machinga ya kuvamia maeneo yasiyo rasmi ikiwamo kando kando ya barabara na kwenye mitaro ya kupitisha maji na kusababisha adha kwa watumiaji wengine.
Alisema halmashauri imetenga barabara zinazotumika kama soko la muda lakini si barabara zote.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara hao kushirikiana na halmashauri ya jiji pale wanapogundua kuna baadhi yao wamekuwa wakikiuka maagizo ili wachukuliwe hatua.
“Pia kuna utapeli kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaowalaghai wenzao kwa kuwauzia maeneo ambayo yapo wazi huku wakidai kuwa wana vibali halali toka halmashauri ya jiji jambo ambalo si la kweli,” alisema.
Chanzo: www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.