Vitambulisho vilivyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama 'wamachinga' vimetolewa kwa wafanyabiashara hao jijini Dodoma.
Akizindua ugawaji wa vitambulisho hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi ametoa vitambulisho 500 kwa wafanyabiashara ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuiletea maendeleo Tanzania.
"Serikali inatambua wapo watu wengi waliojiajiri na kwa kuzingatia hilo Mhe. Rais Magufuli akaona sasa ni vizuri aandae utaratibu rasmi wa kuwatambua wafanyabiashara wote wadogo, hivyo tufanyeni kazi ili tusimuangushe Rais wetu mpendwa" alimeeleza Katambi.
Mkuu wa Wilaya Patrobas Katambi akitoa kitambulisho kwa mmoja wa wafanyabiashara wadogo wa Jiji la Dodoma katikati ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji Gratian Mwesiga.
"Kwa hiyo kwa Jiji letu la Dodoma ni marufuku baada ya muda tuliojipangia kufanya biashara katika jiji letu bila kuwa na kitaambulisho hiki ambacho Mhe. Rais Magufuli kakitoa kwa upendo mkubwa" amesema DC Katambi.
Akiongea katika uzinduzi huo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Graian Mwesiga amewataka wafanyabiashara hao kutumia fursa hii adhimu kukuza mitaji yao na kuleta tija katika biashara zao. Vitambulisho hivi vitumike kuleta chachu ya maendeleo kwa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi. Aidha amesema Halmashauri ya Jiji itaendelea kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara hao kwa mustakabali wa maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Wafanyabiashara hao wamemshukuru Rais Magufuli kwa upendo aliouonesha kwa kuwathamini na kuwapa kipaumbele huku wakimsifu DC Katambi na Mkurugenzi wa Jiji kwa utaratibu bora walioupanga katika kuhakikisha kila machinga anapata kitambulisho.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Patrobas Katambi (mwenye suti nyeusi waliokaa) akiwa na mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya (aliyekaa kulia), Afisa Tarafa wa Dodoma Mjini Neema Nyelege wa pili kushoto walikaa na Mweka Hazina wa Jiji Alfred Mlowe (wa kwanza kushoto waliokaa) kwa pamoja wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo waliopewa vitambulisho vilivyotolewa na Mhe. Rais Magufuli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.