Timu ya madaktari bingwa wa hospitali ya Benjamin Mkapa kutoka Dodoma, inatarajiwa kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya njia ya mkojo, pua, koo na masikio ikiwemo watoto na mifupa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kuanzia Jumatatu Februari 17.
Huu ni mwendelezo wa utoaji Huduma Tembezi "outreach" inayofanywa na hospitali hiyo ikilenga kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi. Mwezi uliopita walikuwa Wilayani Kiteto mkoani Manyara ambako walitoa huduma za magonjwa ya moyo, upasuaji, njia ya mkojo na figo.
Kiongozi wa jopo la madaktari bingwa watakaotoa huduma mkoani Iringa Daktari Charles Lema, amesema kuwa watatoa huduma kwa siku 5. "Kwa hiyo tuwaombe wananchi wa Iringa na maeneo ya jirani, kuchangamkia hiyo fursa, kutakuwa na madaktari bingwa wa mifupa, madaktari bingwa wa magonjwa ya njia ya mkojo, madaktari bingwa wa magonjwa ya pua, koo na masikio, na madaktari bingwa wa watoto" amesisitiza Dkt. Lema.
Aidha, daktari huyo amesema kuwa watatumia fursa hiyo kutambulisha huduma zinazotolewa na Hospitali ya Benjamini Mkapa, ili kama kuna mtu anazihitaji asisite kufika na kupata huduma hizo. Huu ni mwendelezo wa mkakati wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwafikia wananchi, tumetoka Kiteto na tutazidi kwenda maeneo mengine kadiri uhitaji utakavyokuwa unaonekana.
Akitoa ushuhuda wa huduma hizo, Hawa Rajabu mkazi wa Ngarenoro, amesema kuwa "Kwa wamama kama sisi tunashida za matumbo, lakini kama hivyo unaweza ukaenda mahali, wengine wanatumia hata mizizi. Lakini kutokana na madaktari waliokuja kwa utaalam wao tunavyowaeleza kwa kweli wanatusaidia tunashukuru kwa hilo. Tunaomba isiwe mara moja tu, waongeze ili wakati mwingine kwa mwaka iwe mara mbili au mara tatu ili wananchi waweze kusaidika zaidi."
Kwanza natoa shukurani kwa ujio wa madaktari hawa tunashukuru sana, maoni yangu nilikuwa napenda wawe wanatujia mara kwa mara kwa sababu hapa huduma zetu ni chache, huduma zinapatikana lakini nyingi si kama hivi ambazo tumezipata. Tunawashukuru sana hawa madaktari bingwa, watuijie mara kwa mara" amesema mkazi wa Kiteto Zubeda Hasan.
Jopo la madaktari bingwa wakiwa kazini wakati wakihudumia wananchi wa Kiteto.
Chanzo: maelezo tv online
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.