HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma kwa mara nyingine imeandika historia, kwa madaktari wazawa peke yao kufaulu kupandikiza figo kwa ufanisi mkubwa. Madaktari hao wamefaulu kupandikiza figo kwa Emmanuel Kahigi, ambaye kwa miaka mitano hakuwahi kupata mkojo kutokana na figo yake kushindwa kufanya kazi.
Anakuwa mgonjwa wa 12 kupandikizwa figo BMH. Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, Dkt. Alphoce Chandika akizungumza hospitalini hapo jana alisema upandikizaji huo umefanyika Machi 3, mwaka huu kwa ufanisi mkubwa na madaktari wazawa, ambao ni wa kwanza kufanywa na wazawa hospitali hapo na hapa nchini.
“Upandikizaji huo ni wa tano lakini wa kwanza kufanyika na madaktari wazawa wakati ule wa kwanza Machi 2018, wa pili Septemba 2018, wa tatu Agosti 2019 na wa nne Januari 2020 ulifanyika kwa ushirikiano baina ya madaktari bingwa wa Tanzania na taasisi mbili za Japan (Tokushukay Medical Corporation na Taasisi ya Wanawake wa Chuo Kikuu Japan),” alisema Dkt. Chandika.
Dkt. Chandika alisema upandikizaji wa figo kwa Kahigi wa Geita, ulifanyika kwa saa 10.30 ambapo utoaji figo kwa njia ya upasuaji ulifanyika kwa saa 5.30. Upandikizaji ulitumia saa 5.00 na ulikuwa na ufanisi mkubwa kutokana pia na umakini wa watalaamu wa dawa za usingizi.
“Upandikizaji huo unaofanyika kwa ushirikiano wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Benjamin na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ulifanikiwa kutokana na mafunzo ya umahiri waliopata kutoka kwa madaktari wa Japan waliokuja nchini na wale waliokwenda nchini huko,” alisema.
Alisema upandikizaji figo nchini, umepunguza gharama za wagonjwa kwenda India, ambako mgonjwa mmoja hupandikizwa kwa Sh milioni 100, gharama ambazo hospitalini hapo wanatibiwa wagonjwa wanne hadi watano. Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Masumbuko Mwashambwa alisema walifanya upasuaji kwa saa 10.30 kutokana na madaktari wazawa kufanya kwa mara ya kwanza, hivyo walikuwa na tahadhari kubwa.
Dkt. Mashambwa ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, alisema pia walitumia muda mrefu kutokana na shida ya mtoaji figo kuwa na matatizo kwenye mshipa mmoja ambao ni muhimu katika kutoa figo. Pia alizitaka pia hospitali nyingine kama KCMC, Bugando na Mbeya kuiga BMH na kuanzisha huduma hizo za kupandikiza figo kutokana na matatizo hayo kuwa makubwa katika jamii.
Daktari wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Kessy Shija alisema upasuaji huo kufanyika hospitalini hapo, umesaidia kupunguza gharama, ambazo angetumia kwenda kufanyiwa upandikizaji nje ya nchi. Dkt. Shija pia alipongeza timu ya wapandikizaji figo, ambao walionesha umahiri wa hali ya juu katika kuhakikisha mgonjwa anayepandikizwa figo, anakuwa salama pamoja na mtoaji.
Chanzo: Tovuti ya HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.