HAMASA imetolewa kwa wachimbaji wadogo wa Madini wa Mkoa wa Dodoma kuifanya sekta hiyo kuakisi uchumi wa wananchi wa Dodoma kwani ndio Mkoa pekee nchini ambao unapatikana aina nyingi zaidi za madini ukilinganishwa na Mikoa mingine ya Tanzania.
Hayo yalibainishwa lwakati wa kikao kazi kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule na wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wakala wa utafiti wa madini (GST), STAMICO, Tume ya madini pamoja na wachimbaji wadogo wa madini ndani ya Mkoa wa Dodoma. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa.
"Natamani madini yaonekane kwenye sura za wananchi wa Dodoma ili yachechue Uchumi wa wananchi na Mkoa kwa ujumla. Mhe. Rais ameipa kipaumbele sekta ya madini kwa kuboresha sera mbalimbali za madini kama vile kuimarisha kodi, ushuru pamoja na utafiti.
" Mkoa pia katika vipaumbele vyake umeipa madini kuwa kipaumbele namba moja ikifuatiwa na viwanda, Utalii, Mji wa kimkakati n.k. sekta hii imepewa uzito Mkubwa kwa kupewa thamani ya kubadilisha maisha ya watu.Tunatamani Dodoma tuwe wanufaika wa madini haya" Alisema Senyamule.
Awali akitoa taarifa ya utafiti wa madini yanayopatikana ndani ya Mkoa wa Dodoma, Mjiolojia kutoka GST Bw. Abbas Mruma, amesema Mkoa wa Dodoma unashika namba 1 kwa kuwa na aina nyingi za madini ukifuatiwa na Mkoa wa Lindi kwa kuwa unapatikana kwenye makutano ya miamba mikubwa ambayo ina miaka mingi zaidi ya 300 na kadri umri wa mwamba unavyokua mkubwa, ndivyo unavyozidi kuwa imara na kutoa madini imara pia.
"Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa upatikanaji wa madini aina 47 huku Lithium ikiongoza tena yenye ubora ikipatikana kwenye eneo la Hombolo Jijini Dodoma na kufuatiwa na madini mengine kama vile Dhahabu, Nikel, Shaba, chuma, Uranium na mengine mengi. Tafiti zinaonesha kuwa uchimbaji mkubwa wa madini ulifanyika kwenye Mlima Sekenke huko Singida kwa madini ya Dhahabu lakini pia tumegundua kuna uwiano wa takribani madini 100,000 ardhini kwa nchi nzima ikiwemo Dodoma" Ameongeza Bw. Mruma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.