Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutafsiri kwa vitendo maana ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kubadilisha maisha ya watu na kuyafanya kuwa bora kuliko jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati akifungua mkutano wa Baraza la Madiwani wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji kutoka kwenye kata kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili-Juni, 2024) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Prof. Mwamfupe ambae pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “hakuna ubishi wowote jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyopeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mengi ya Jiji la Dodoma. Penye ubishi ni pale tunaposhindwa kutafsiri miradi hii kwenye maisha ya watu ya kila siku. Lazima tuongelee jinsi mwananchi wa kawaida alivyosaidika na miradi hii. Mfano, treni ya SGR ilikuwa ni ndoto, lakini juzi ilivyozinduliwa ilikuwa ni halisi. Kazi yetu wanasiasa ni kuelezea mwananchi anavyonufaika”.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wendo Kutusha alitoa shukrani kwa halmashauri kutekeleza miradi mingi ya maendeleo. Aidha, alishauri ushirikiano baina ya Divisheni ya elimu na watendaji wa kata katika kudhibiti utoro wa wanafunzi katika baadhi ya maeneo ili kuongeza ufaulu.
Wakati huohuo, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asma Karama aliishukuru serikali kwa kutoa fedha nyingi Jiji la Dodoma. “Napenda kumshukuru Mheshimima Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa jicho la huruma na kutupatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo” alisema Karama.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.