Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MADIWANI na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kuungana kukusanya mapato ya serikali ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyopitishwa katika rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko alipokuwa akichangia rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwaluko alisema kuwa kupanga bajeti ni kitu kimoja na utekelezaji ni kitu kingine. “Waswahili wanasema kidole kimoja hakivunji chawa. Ili twende tukaitekeleza bajeti hii vizuri ndugu madiwani na wataalam twende tukaungane ili tuweze kukusanya mapato yatakayoweza kutekeleza bajeti hii ambayo ni nzuri sana. Hatutaweza kutekeleza miradi ya maendeleo bila kuwa na mapato yatakayoeleweka. Twendeni tukasimamie watendaji wetu kwenye kata na sisi tusimamie ukusanyaji wa mapato wa Jiji la Dodoma ili tufanye vizuri” alisisitiza Mwaluko.
Vilevile, alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Jiji la Dodoma miradi mbalimbali ya maendeleo. “Kingine nitakuwa mchoyo wa fadhira nisipomshukuru Rais. Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ameweza kutupendelea kwelikweli. Tuna miradi mikubwa katika sekta mbalimbali ambazo mkono wake umekuwa mrefu sana katika miradi hiyo mkubwa ikiwemo sekta ya afya na kipekee sekta ya elimu. Tumeona jinsi shule ambavyo zimejengwa kwa kasi na vifaa kwa ajili ya elimu na afya” alisema Mwaluko.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.