Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi katika kata zao bila kusubiri vikao vya maamuzi.
Maelekezo hayo yalitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani alipokuwa akichangia hoja katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema “msisitizo mkubwa kwetu madiwani ambao tunatakiwa kuukwepa ni pale tunaposhindwa kutenganisha masuala ya utendaji wa kila siku na masuala ya kimipango yanayohitaji maamuzi. Baraza hili lisingekuwa sehemu ya kusema mtendaji wangu amenikwaza, tuyaseme hayo yanapokuwa matatizo sugu. Yale matatizo ya kiutendaji yasisubiri vikao vya baraza. Utatuzi wa shida za wananchi wetu usisubiri mabaraza. Mabaraza yawe kwa ajili ya kufanya maamuzi”.
Akitoa salamu zake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alimpongeza mwenyekiti wa mkutano huo ambaye ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuendesha Baraza la Madiwani kwa weledi. “Ufanisi wa baraza hili unaweza kutafsiriwa kwa wakuu wa idara watatu kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri. Hongereni baraza kwa kuwalea vijana hawa” alisema Shekimweri.
Akimuongelea Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu huyo wa wilaya alimtaja kuwa msikivu na muungwana. “Nasaha zangu kwa Mkurugenzi wa Jiji, abaki kuwa Joseph Mafuru. Aishi kwa tabia zake, ni mtu msikivu, muungwana, ana adabu na mtu anayetoa ushirikiano. Ukiyaishi hayo utafanikiwa. Hivyo basi, jenga timu ambayo najua ipo tayari ila badilisha ‘culture’ ya utendaji kazi. Hasa kujibu barua za wananchi. Kujenga tamaduni ya kujali wateja. Huduma kwa mteja ni muhimu sana” alisisitiza Shekimweri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.