WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki amesema maelfu ya Watanzania wanatarajia kunufaika na ajira katika ujenzi wa Kituo cha Kibiashara Afrika Mashariki nchini.
Ujenzi huo unatarajiwa kutoa ajira rasmi 15,000 na zisizo rasmi 50,000 kwa Watanzania.
Aliyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kibiashara Afrika Mashariki katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo,Dar es Salaam.
Alisema, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ilipokea mradi wa uwekezaji wa Ujenzi wa Kituo cha Kibiashara Afrika Mashariki mwaka 2021 kutoka kwa iliyokuwa Jiji la Dar es Salaam katika eneo la iliyokuwa stendi ya mabasi ya Ubungo. "Mkataba wa awali wa uwekezaji ulisainiwa mwaka 2015 kati ya Jiji la Dares salaam na Mwekezaji Shanghai Linghang Group Limited ambapo mpaka Manispaa ya Ubungo inapokea mradi huu, utekelezaji ulikuwa bado haujaanza.
"Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi ya Uwekezaji Tanzania iliunda kikosi kazi kwa ajili ya kupitia Mkataba wa awali na kuishauri Manispaa ya Ubungo.
"Baada ya Kikosi kazi kutekeleza wajibu wake iliishauri Manispaa ya Ubungo kupangisha eneo hilo na kusaini Mkataba na mwekezaji, ambao ulisainiwa tarehe 16/12/2022 kati ya Manispaa ya Ubungo na Shanghai Linghang Group Limited,"amefafanua Mheshimiwa Kairuki.
Pia, amesema uwekezaji katika eneo la Ubungo una thamani ya dola za Kimarekani 81,827,655.01 na ni mkataba wa miaka 32 tangu kusainiwa ambapo mwekezaji atakuwa amerejesha fedha za uwekezaji na kutakiwa kukabidhi umiliki kwa Manispaa ya Ubungo.
"Mradi huu utaifungua Tanzania kibiashara na kukuza uchumi kutokana na biashara zitakazokuwa zikifanyika na kukuza mahusiano ya Kimataifa kwa kuwa na muingiliano wa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali,"alisema.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.