Naibu Waziri wa Maliasiri na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuyatumia magari 14 waliyokabidhiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Kusini.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akikabidhi magari 14 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi na Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akifafanua zaidi Naibu Waziri huyo amesema kupatikana kwa magari hayo katika Mradi wa REGROW ni muendelezo na jitihada za Serikali za kuhakikisha shughuli za Utalii zinafanyika kanda zote za nchi na sio ukanda wa Kaskazini pekee kama ilivyo sasa.
"Hatusemi kuwa Kaskazini inapendelewa bali tunataka kuona watalii wanatembelea vivutio vya utalii katika kona zote za nchi yetu na hii tutafanikiwa kwa kuimarisha miundombinu" amesisitiza Kanyasu.
Katika hatua nyingine Mhe. Kanyasu amelitaka TANAPA kuyatumia magari hayo kuboresha ujirani mwema kwa jamii zinazoishi karibu na Hifadhi kwa lengo la kufanya jamii hizo ziweze kushiriki katika shughuli za utalii pamoja na ulinzi wa wanyamapori.
Aidha, ametaka magari hayo kusaidia kuimarisha utendaji wa Hifadhi za Taifa katika ulinzi pamoja na kuwahudumia watalii pamoja na kusaidia katika shughuli za ujirani mwema.
Mradi wa REGROW unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na baadhi ya Taasisi zake ambazo ni TANAPA, NCAA, TTC na TAWIRI.
Baadhi ya magari yaliyokabidhiwa kwa ajili ya kukuza utalii ukanda wa Kusini mwa Tanzania.
Chanzo: Ukurasa wa Wizara ya Maliasili na Utalii - wizarayamaliasilinautalii - instagram
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.