WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ameelekeza magari yote ya wagonjwa nchini yaliyotolewa na Serikali yanakatiwa Bima ya ajali ili iweze kusaidia katika matengenezo pale yanapopata ajali au kuharibika.
Mwalimu amesema hayo jijini Dodoma wakati akikabidhiwa magari 8 ikiwemo gari la wagonjwa yenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika ambayo yatatumika katika kujenga uwezo wa nchi wa kujiandaa,kugundua na kukabiliana na maafa na majanga ya afya ya jamii.
Mwalimu ameonekana kusikitishwa na taarifa za kuharibika kwa magari ya wagonjwa ambayo yametolewa na Serikali katika Halmashauri mbalimbali nchini ili yaweze kutoa huduma kwa wagonjwa wa maeneo husika lakini inakua tofauti na matarajio yaliyokusudiwa kwani mengi yanapata ajali au kuharibika na kuachwa bila matengenezo.
“Naumia sana kuona magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) tuliyonunua kwa bei kubwa yanakua hayakatiwi Bima na matokeo yake yakipata ajali au kuharibika yanatekelezwa. Kwahiyo nataka 'Ambulance' zote nchini zilizotolewa na Serikali zikatiwe Bima”. Amesisitiza Mwalimu.
Aidha, Mwalimu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuandaa mafunzo kwa madereva watakaoendesha magari hayo yaliyotolewa na WHO kuwa na mwitikio wa dharura katika majanga ya kiafya na ajali ili kuweza kukabiliana na maafa kwa haraka na kuweza kuokoa Maisha.
Pamoja na hayo Mwalimu amelishukuru Shirikia la Afya Duniani (WHO) kupitia kwa Kaimu Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania Dkt. Zabulon Yoti kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kutoa vifaa ikiwemo magari hayo ili kuweza kuimarisha hali ya utayari wa nchi katika kukabiliana na dharura na majanga ya afya ya jamii.
Mwisho, Mwalimu ameendelea kusisitiza ushiriki wa Sekta zote muhimu nchini katika kupambana na kukabiliana na majanga yanayoathiri afya ya jamii kwani hayahusu sekta ya afya peke yake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.